NA DIRAMAKINI
SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limetangaza kurejea rasmi kwa huduma za usafiri wa abiria kwa kutumia treni za reli ya kiwango cha mita (MGR) kuelekea mikoa ya Kigoma, Mwanza, Moshi na Arusha kuanzia Juni 18, 2026, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za usafiri na kukidhi mahitaji ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Juni 12,2026 na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa TRC, Fredy Mwanjala.
Ratiba mpya imeandaliwa ili kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kwa ufanisi na kuendana na ongezeko la mahitaji ya usafiri wa reli.
Katika ratiba hiyo, kutakuwa na safari mbili kwa wiki kuelekea Kigoma zitakazofanyika kila Jumapili na Alhamisi, safari moja kwa wiki kuelekea Mwanza kila Alhamisi, pamoja na safari moja kwa wiki kuelekea Arusha kupitia Moshi kila Ijumaa.
Aidha,kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa, safari ya kwanza itaanza Alhamisi, Juni 18, 2026 saa 2:00 asubuhi ambapo Treni ya Deluxe itaondoka jijini Dar es Salaam kuelekea Kigoma na Mwanza. Safari ya pili itafanyika Ijumaa, Juni 19, 2026 saa 8:30 mchana ambapo Treni ya Deluxe itaondoka Dar es Salaam kuelekea Arusha kupitia Moshi.
Aidha, Jumapili, Juni 21, 2026 saa 9:30 alasiri, Treni ya Ordinary itaondoka Dar es Salaam kuelekea Kigoma, ikiwa ni sehemu ya ratiba mpya ya safari za reli hizo.
TRC imeeleza kuwa uamuzi wa kurejesha huduma hizo umetokana na kuongezeka kwa mahitaji ya usafiri wa abiria katika maeneo mbalimbali ya nchi pamoja na dhamira ya kuboresha huduma za usafiri wa reli kwa wananchi.
Shirika hilo pia limewataka wasafiri kupanga safari zao mapema kwa kukata tiketi kupitia mfumo rasmi wa ukataji tiketi unaopatikana katika stesheni za reli pamoja na mifumo ya mtandaoni ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza kutokana na ongezeko la mahitaji ya tiketi.

