DAR-Mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, Kamishna wa Polisi CP Edwin Abraham Mani umezikwa Julai 18, 2026 nyumbani kwake Bonyokwa, Ilala Dar es Salaam.
Katika kutoa salamu za pole kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Daniel Nyambabe amesema marehemu ameliachia heshima kubwa Jeshi la Polisi. Aliongeza kuwa CP Edwin alifanya kazi kwa weledi mkubwa hadi wakati wa kustaafu kwake.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, Kamishna Mwandamizi wa Polisi SACP Renada Mzinga amesema kuwa ingawa CP Edwin alikuwa amestaafu, alikuwa msaada mkubwa katika kutoa ushauri wa masuala mbalimbali ya kiutendaji ndani ya Jeshi hilo, hasa katika Kamisheni ya Upelelezi.
Aliongeza kuwa marehemu alikuwa mstari wa mbele katika kulinda heshima na weledi wa Jeshi la Polisi na mchango wake katika kupambana na uhalifu ulitambulika.
Maziko hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mh. Edward Mpogolo akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Albert Chalamila. Pia walihudhuria viongozi wa Jeshi la Polisi pamoja na ndugu, jamaa na marafiki.







