DODOMA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeratibu mafunzo kuhusu Dhamana za Serikali kwa wanafunzi wa Shahada ya Uhasibu na Fedha wa Chuo Kikuu cha St John's.
Mafunzo hayo yalifanyika Julai 3, 2026 katika Makao Makuu ya BoT jijini Dodoma, ambapo wanafunzi walipata fursa ya kujifunza namna Benki Kuu inavyoratibu utoaji na usimamizi wa dhamana za Serikali.
Pia, wanafunzi hao walipatiwa elimu kuhusu historia ya Benki Kuu ya Tanzania, majukumu yake ya msingi katika kusimamia sera za fedha, kulinda uthabiti wa mfumo wa fedha na mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa nchi.
Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha St John's, Dkt. George Mkoma, aliipongeza BoT kwa kuendelea kufungua milango yake kwa taasisi za elimu na kuwapa wanafunzi nafasi ya kujifunza kwa vitendo alisema hatua hiyo inawajengea wanafunzi uwezo wa kuunganisha nadharia wanazojifunza darasani na mazingira halisi ya kazi.Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Benki Kuu wa kuifikia jamii kupitia utoaji wa elimu kwa makundi mbalimbali, ikiwamo wanafunzi wa vyuo vikuu, ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu majukumu yake na mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.



