Waziri wa Fedha,Balozi Omar ashiriki Mkutano wa African Caucus wa mwaka 2026

BANJUL-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameongoza ujumbe wa Tanzania katika ufunguzi wa Mkutano wa African Caucus wa Mwaka 2026, jijini Banjul nchini Gambia, uliofunguliwa na Rais wa nchi hiyo Mhe. Adama Barrow, ambapo msisitizo mkubwa umewekwa katika Bara la Afrika kuongeza uwezo wake wa kujitegemea kwa kutumia rasilimali zake lakini pia kuvutia mitaji na uwekezaji kutoka sekta binafsi.
Mkutano huo umewakutanisha wadau wakiwemo viongozi wa Afrika, watunga sera, wataalamu wa fedha, washirika wa maendeleo, kutoka nchi 54 za Bara la Afrika pamoja na wawakilishi wa taasisi za kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Aidha, ujumbe wa Tanzania umemhusisha Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba.
Ufunguzi huo umefanyika katika Kituo cha Mikutano cha SDJK, jijini Banjul, na utakuwa jukwaa muhimu kwa nchi za Afrika kujadili masuala muhimu ya uchumi na maendeleo yanayoikabili Bara la Afrika, pamoja na kuweka msimamo wa pamoja katika kushirikiana na taasisi kubwa za kifedha duniani.

African Caucus ni jukwaa linalowakutanisha magavana wa Afrika katika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia, ambalo huzisaidia nchi za Afrika kuzungumza kwa sauti moja kuhusu masuala kama usimamizi wa madeni, fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, maendeleo ya miundombinu, kupunguza umasikini, kukuza ajira, biashara, na mageuzi ya kiuchumi.
Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, wanatarajiwa kuzungumza katika mkutano huo wa siku tatu ulioanza tarehe 5 hadi 8 Julai, 2026, kuhusu namna Tanzania ilivyojipanga kimkakati kukuza uchumi wake kwa faida ya watu wake na wawekezaji kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here