NA GODFREY NNKO
MKUU wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam,Mheshimiwa Sixtus Mapunda ametoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina katika baadhi ya maeneo ya biashara ya magari maarufu kama showrooms wilayani humo, akisema wingi wa magari ya kifahari yanayouzwa katika baadhi ya maeneo unaibua maswali yanayohitaji majibu.
Mheshimiwa Mapunda amesema uchunguzi huo unapaswa kusaidia kubaini iwapo kuna baadhi ya biashara zinazoweza kutumiwa kuficha au kutakatisha fedha zinazotokana na shughuli haramu ikiwemo biashara ya dawa za kulevya.
Ametoa kauli hiyo Julai 23,2026 katika Viwanja vya Mwembeyanga,Temeke jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Tamasha la Kuwafikia na Kuhamasisha Jamii dhidi ya Dawa za Kulevya, lililoanza kwa matembezi kutoka eneo la Kwa Azizi Ally ambalo limeratibiwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
Amesema,baadhi ya maeneo yanayouza magari ya kifahari, hususan katika maeneo ya Kiburugwa na Buza yanaonekana kuwa na magari mengi ya gharama kubwa, hali ambayo, kwa mtazamo wake inapaswa kuchunguzwa ili kubaini uhalali wa biashara hizo na vyanzo vya fedha zinazotumika.
“Haiwezekani kuona magari ya kifahari yanauzwa Kiburugwa au Buza, tena yakiwa lukuki. Ni kweli mtu anaweza kuja Temeke kununua magari hayo? Natoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuzichunguza showrooms hizo ili kubaini ukweli,”amesema.
Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza kuwa kauli hiyo haimaanishi kuwa kila mfanyabiashara wa magari ya kifahari anahusika na uhalifu, bali ameeleza umuhimu wa kufanya uchunguzi wa kisheria pale ambapo kuna viashiria vinavyoweza kuibua maswali kuhusu chanzo cha mali au fedha zinazotumika katika biashara.
Amesema,vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kuchunguza kwa kina vyanzo vya utajiri usioelezeka pamoja na biashara zinazoweza kutumiwa kutakatisha fedha zinazotokana na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Vijana waonywa
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Mapunda amewataka vijana kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya, akisema madhara yake huanza taratibu na baadaye kuharibu afya, maisha na mustakabali wa mtumiaji.
Amesema,dawa za kulevya zinaweza kumvuta mtu hatua kwa hatua, kuanzia majaribio hadi kufikia utegemezi mkubwa unaoweza kufanya iwe vigumu kurejea katika maisha ya kawaida.
Amesema,vita dhidi ya dawa za kulevya inahitaji kukata njia za usambazaji, kuzuia biashara haramu na, muhimu zaidi kupunguza idadi ya watumiaji kwa sababu bila mahitaji, biashara hiyo itakosa soko.
Mheshimiwa Mapunda amewataka wazazi kuanza kuwapa watoto elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya tangu wakiwa wadogo ili kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi wanapokua.
Pia amewataka vijana kutofuata mkumbo wa kujaribu kila jambo kwa kisingizio cha fasheni au ushawishi wa marafiki, akisisitiza kuwa matumizi ya dawa za kulevya yanaweza kuanza kwa majaribio lakini baadaye kugeuka kuwa utegemezi.
Aidha, amekemea tabia ya baadhi ya watu kuonesha utajiri uliopitiliza kupitia mitandao ya kijamii, wakiweka picha za fedha nyingi, magari ya kifahari na maisha ya anasa bila kueleza chanzo cha mali hizo.
Amesema,hali hiyo inaweza kuwavutia vijana kutafuta utajiri wa haraka kwa njia zisizo halali, wakiiga maisha ya watu ambao huenda wameyafikia kwa kutumia njia za uhalifu.
Temeke ina waraibu 2,500 wanaotumia methadone
Kwa upande wake, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema Wilaya ya Temeke inaongoza kwa idadi ya waraibu wa dawa za kulevya wanaopata huduma za tiba ya methadone katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa DCEA, Kamishna Msaidizi wa Tiba na Huduma za Utengamao, Dkt. Cassian Nyandindi amesema,jumla ya watu 2,500 waliokuwa wakitumia dawa ya kulevya aina ya heroin wanapata huduma ya methadone katika Wilaya ya Temeke.
Amesema,idadi hiyo ni kubwa kwa kiwango cha wilaya na inaonesha ukubwa wa changamoto ya matumizi ya dawa za kulevya katika eneo hilo.
“Tatizo la dawa za kulevya ni kubwa Dar es Salaam kwa wilaya zote, lakini Temeke inaongoza kwa kuwa katika eneo hili tatizo ni kubwa. Watu 2,500 waliokuwa wakitumia heroin wanatumia huduma ya methadone, na hiyo ni idadi kubwa kiwilaya,”amesema Dkt. Nyandindi.
Amesema, mbali na huduma ya methadone, takribani watu 16,000 walipatiwa huduma za afya ya akili katika Wilaya ya Temeke mwaka 2014.
Dkt.Nyandindi amesema,matamasha ya uhamasishaji ni muhimu kwa sababu yanaifanya jamii kutambua ukubwa wa tatizo na kuelewa kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya si jukumu la mtu mmoja, bali ni wajibu wa jamii nzima.
Amesema,tatizo la dawa za kulevya haliwezi kumuacha mtu yeyote salama, kwa kuwa hata kama halimgusi mtu moja kwa moja, linaweza kumuathiri mwanafamilia, jirani au jamii kwa ujumla.
DCEA imesema matamasha ya uhamasishaji pia hufanyika katika kanda mbalimbali nchini, ikiwemo Kanda ya Mashariki, Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kusini.
Temeke ni eneo linaloweza kutumiwa kusambaza dawa za kulevya
Vilevile,akizungumza katika tamasha hilo, Mheshimiwa Mapunda amesema jiografia na mazingira ya Wilaya ya Temeke yanaweza kurahisisha matumizi na usambazaji wa dawa za kulevya, hali inayohitaji wananchi kupewa elimu na kushirikishwa kikamilifu katika mapambano hayo.
Amesema,tatizo hilo ni kubwa na madhara yake yanaweza kuchukua muda mrefu kuonekana, huku baadhi ya waathirika wakifikia hatua ambayo kupona huwa changamoto.
Amesema,njia mojawapo ya kukabiliana na tatizo hilo ni kukata mnyororo wa usambazaji na kupunguza idadi ya watumiaji.
“Kuna ugumu wa kukata usambazaji kwa sababu hauna njia moja wala fomula moja. La pili ni kupambana na yule anayeenda kutumia, kwa sababu tusipokuwa na watumiaji, mzigo hautafika. Tukikata watumiaji, mzigo hautafika mtaani kwa sababu utakuwa hauna soko,” amesema.
Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa wazazi kuzungumza na watoto wao mapema kuhusu dawa za kulevya na madhara yake.
Amesema watoto wanapaswa kufundishwa kuwa si kila jambo ni la kujaribu, hasa mambo yanayoweza kuwaweka katika utegemezi na kuharibu maisha yao.
Mraibu aliyepata nafuu asimulia safari ya miaka 13
Naye mmoja wa waliowahi kutumia dawa za kulevya na baadaye kupata nafuu, Sura Nyembo amesema, alianza kutumia heroin mwaka 2000 na kuacha mwaka 2013 baada ya kupata msaada kupitia nyumba za upataji nafuu.
Nyembo amesema alitumia heroin kwa takribani miaka 13, hali iliyomfanya akabiliwe na changamoto mbalimbali katika maisha yake, ikiwemo kuathirika kwa masomo.
“Nimetumia heroin kwa miaka 13. Kupitia nyumba hizi za kujitibu nilibahatika kuondokana na matumizi haya. Jamii inatakiwa kujua dawa za kulevya si kitu kizuri. Mimi niliacha hadi masomo,”amesema.
Amesema, ili kukabiliana na tatizo hilo, ni muhimu kupunguza idadi ya watumiaji kwa kutoa elimu, huduma za tiba na msaada wa kijamii, kwa kuwa kupungua kwa mahitaji kutasaidia kupunguza soko la dawa za kulevya na hatimaye kudhoofisha mtandao wa usambazaji.
Nyembo pia amesema pamoja na matumizi ya heroin na dawa nyingine za kulevya, kumekuwa na ongezeko la matumizi ya bangi aina ya skanka, hali ambayo amesema inahitaji uelewa na hatua zaidi za pamoja kutoka kwa Serikali, wazazi na jamii.
Tamasha hilo la DCEA lililenga kuhamasisha jamii kushiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kupitia elimu, ushirikiano na utoaji wa taarifa kwa mamlaka husika.
Mamlaka imeendelea kusisitiza kuwa, mafanikio katika mapambano hayo yatategemea ushirikiano wa wananchi, wazazi, taasisi za Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wadau wengine katika kukataa matumizi, kuzuia biashara na kutoa taarifa kuhusu usambazaji wa dawa za kulevya.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Makala
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)





























