Dhahabu ya Shilingi bilioni 1.2 yakamatwa ikitoroshwa

DAR-Serikali kupitia Wizara ya Madini imekamata dhahabu yenye uzito wa gramu 4,402.20 na thamani ya Shilingi 1,238,458,594.42, iliyokuwa ikitoroshwa nje ya mfumo rasmi wa biashara ya madini nchini.
Tukio la utoroshaji wa madini hayo limetokea Julai 25,2026 katika eneo la Kiluvya lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani.

Hatua hiyo ni sehemu ya operesheni zinazoendelea kufanywa na Kikosi Kazi (Taskforce) kilichoanzishwa na Wizara ya Madini kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, kwa lengo la kudhibiti biashara haramu ya madini na vitendo vya utoroshaji wa madini.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo Julai 27,2026, Waziri wa Madini,Mheshimiwa Anthony Mavunde amesema,kukamatwa kwa dhahabu hiyo ni miongoni mwa matokeo ya kuimarishwa kwa mfumo wa udhibiti wa biashara ya madini nchini.

Amesema,dhahabu hiyo yenye thamani ya zaidi ya Sh1.2 bilioni haikupitia katika mfumo rasmi wa biashara ya madini, hali ambayo ingeisababishia Serikali kukosa mapato muhimu kwa ajili ya kugharamia huduma za maendeleo kwa wananchi.

“Serikali kupitia Wizara ya Madini iliunda Kikosi Kazi ambacho kinahusisha vyombo vya dola ili kudhibiti biashara haramu ya madini na utoroshaji. Hii ni sehemu tu ya kazi ambazo zimeendelea kufanywa na Kikosi Kazi hicho katika kuimarisha mfumo wa ufanyaji biashara ya madini,"amesema Mavunde.

Amesisitiza kuwa,madini hayo yamekamatwa kwa kuwa yalikuwa yakisafirishwa nje ya mfumo rasmi wa biashara unaotambuliwa na Serikali.

“Dhahabu hii yenye zaidi ya thamani ya bilioni 1.2 haikupitia katika mfumo rasmi wa ufanyaji biashara ya madini na hivyo kupelekea Serikali kukosa mapato ambayo yangeisaidia kuimarisha utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi,” amesema.

Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, dhahabu hiyo imechukuliwa na Serikali kwa mujibu wa taratibu za kisheria na tayari imehifadhiwa katika Benki Kuu ya Tanzania.

Aidha, amekiagiza Kikosi Kazi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola kufanya mahojiano ya kina kwa mtuhumiwa aliyekamatwa akiwa na dhahabu hiyo, ili kubaini chanzo cha madini hayo pamoja na yalipokuwa yakipelekwa.

Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kubaini na kuvunja mnyororo mzima wa mtandao wa utoroshaji wa madini, badala ya kumaliza kwa kumkamata mtu mmoja aliyebainika akiwa na madini hayo.

Waziri Mavunde pia ameelekeza kuwa, iwapo mtuhumiwa huyo alikuwa na leseni ya kufanya biashara ya madini, leseni hiyo ifutwe mara moja kwa mujibu wa sheria na jina lake liingizwe katika orodha maalum ya wafanyabiashara waliokiuka sheria (blacklist), ili asiruhusiwe tena kufanya biashara ya madini nchini.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amewataka wananchi kuzingatia sheria na kutumia mifumo rasmi ya biashara ya madini iliyowekwa na Serikali, ikiwemo masoko ya madini na vituo vya ununuzi vilivyoanzishwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema,matumizi ya mifumo hiyo ni muhimu katika kuhakikisha Serikali inapata mapato stahiki kutokana na rasilimali za madini, huku wafanyabiashara wakifanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.

Waziri Mavunde amesisitiza kuwa, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini na kuchukua hatua dhidi ya watu wanaojihusisha na biashara haramu, utoroshaji na ukiukwaji wa taratibu za biashara ya madini, kwa lengo la kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha Watanzania wote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here