NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema, kalamu ya Mwanasheria wa Serikali ni nyenzo muhimu katika kulinda maslahi ya Taifa, akisisitiza kuwa ikitumika kwa weledi, uadilifu na uzalendo inaweza kuzuia hasara kwa Serikali kabla hazijatokea, kuhakikisha maamuzi sahihi yanafanyika na kuchochea maendeleo endelevu ya nchi.
Ameyasema hayo leo Julai 13,2026 wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) unaofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) jijini Arusha.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais Dkt.Samia amesema tofauti na kalamu yake ambayo hutumika katika hatua za mwisho za utekelezaji wa sheria, kalamu ya Mwanasheria wa Serikali ina nafasi ya kipekee ya kuzuia migogoro,hasara na makosa ya kisheria kabla hayajatokea kupitia ushauri wa kitaalamu unaolinda maslahi ya Taifa.
"Kalamu ya Mwanasheria wa Serikali ikitumika kwa weledi na uaminifu inaweza kuzuia hasara kwa Serikali kabla hazijatokea na kusaidia kufanyika kwa maamuzi sahihi yenye manufaa kwa wananchi."
Pia,amewataka mawakili wa Serikali kutekeleza wajibu wao kwa uadilifu,uzalendo na uaminifu, wakitanguliza maslahi ya Taifa badala ya maslahi binafsi, huku wakihakikisha sheria zinatumika kwa haki na zinachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Rais Dkt.Samia amesema,sekta ya sheria ina nafasi kubwa katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akieleza kuwa sheria bora, mikataba imara na taasisi zenye uwajibikaji ndizo msingi wa kujenga uchumi shindani, jumuishi na unaovutia uwekezaji.
Amesisitiza kuwa,Serikali itaendelea kuwekeza katika kuwawezesha mawakili wa Serikali kwa kuwajengea uwezo wa kitaaluma,kuboresha mazingira ya kazi na kuimarisha taasisi za sheria ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
"Wakati Serikali inaendelea kuwajengea uwezo na kuboresha mazingira ya kazi, ni muhimu taaluma yenu isitumiwe kwa nia ovu dhidi ya Taifa. Chama hiki kiendelee kuwa chombo cha kujenga weledi,maadili,nidhamu na ubunifu kwa manufaa ya nchi."
Rais Dkt.Samia pia amewapongeza mawakili na maafisa sheria wa Serikali kwa mchango wao katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria na kliniki za sheria pamoja na juhudi za kutafsiri sheria kwa lugha ya Kiswahili, hatua inayosaidia wananchi kuelewa haki, wajibu na misingi ya utawala wa sheria.
Amesema,hatua hizo zimekuwa muhimu katika kuimarisha imani ya wananchi kwa mfumo wa haki na kuongeza upatikanaji wa huduma za kisheria kwa makundi mbalimbali ya jamii.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt.Samia amemtaka Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera kushughulikia changamoto zilizowasilishwa na Chama cha Mawakili wa Serikali, akibainisha kuwa baadhi ya changamoto hizo tayari zimeanza kutafutiwa ufumbuzi, ikiwemo upatikanaji wa ofisi na viwanja kwa ajili ya chama hicho katika miji ya Dodoma na Arusha.
Kabla ya kufungua rasmi mkutano huo, Rais Dkt.Samia alipokea nakala ya kitabu "Mama Samia Doctrine of Law (Falsafa ya Sheria ya Mama Samia)" kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari.
Kitabu hicho kinaelezea falsafa ya uongozi wa Rais Dkt.Samia, historia yake pamoja na hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kuimarisha utawala wa sheria, kufanya mageuzi ya taasisi za umma na kuharakisha maendeleo ya Taifa kupitia misingi ya sheria.
Katika hafla hiyo, Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) kimemtunuku Rais Dkt.Samia Tuzo ya Heshima kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha utawala wa sheria, sekta ya sheria na utoaji wa haki nchini. Tuzo hiyo ilikabidhiwa na Rais wa TPBA, Bw. Bavoo Anatoly Junus, mbele ya mamia ya washiriki wa mkutano huo.
Aidha,kabla ya hafla ya ufunguzi, Rais Dkt. Samia alitembelea mabanda ya maonesho ya taasisi mbalimbali za sekta ya sheria yaliyokuwa yakionesha huduma, ubunifu na mafanikio yaliyofikiwa katika kuboresha utoaji wa huduma za kisheria nchini.
Mkutano Mkuu wa TPBA wa mwaka huu unajadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya taaluma ya sheria, matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za kisheria, uimarishaji wa uwezo wa mawakili wa Serikali pamoja na kubadilishana uzoefu kuhusu changamoto na fursa zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kupitia mkutano huo, Serikali imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kujenga taasisi imara za haki, kuimarisha utawala wa sheria na kuhakikisha sekta ya sheria inaendelea kuwa nguzo muhimu katika kulinda maslahi ya Taifa na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Tags
Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania
Dr Samia Suluhu Hassan
Falsafa ya Sheria ya Mama Samia
Habari
Mwanasheria Mkuu wa Serikali










