KIGOMA-Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, amesema ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha sita kutoka Tabora hadi Kigoma ni hatua ya kimkakati itakayoiunganisha Tanzania na masoko ya ukanda wa Maziwa Makuu kupitia mtandao wa kisasa wa reli.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Mkuu wa Mkoa Kigoma kuelekea uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo, Prof. Mbarawa amesema reli hiyo yenye urefu wa kilomita 506 na thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 2.74 itaunganisha Kigoma na mikoa ya Tabora, Shinyanga, Mwanza, Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam, huku ikiimarisha usafirishaji wa mizigo na abiria ndani na nje ya nchi.
Aidha, amesema kukamilika kwa mradi huo kutapunguza muda wa safari kati ya Dar es Salaam na Kigoma kutoka takribani saa 30 zinazotumika sasa kwa reli ya MGR hadi saa nane pekee kwa SGR, pamoja na kuandaa mazingira ya kuunganisha Tanzania na Burundi pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupitia mtandao wa reli wa kikanda.
Prof. Mbarawa amewataka wananchi kuendelea kuunga mkono na kulinda mradi huo, akieleza kuwa SGR ni nguzo muhimu ya kukuza biashara, uwekezaji na maendeleo ya uchumi wa Taifa na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.






