NA DIRAMAKINI
MAHAKAMA nchini China imemhukumu adhabu ya kifo aliyekuwa kiongozi mwandamizi wa Jiji la Nanjing, Yang Youlin baada ya kupatikana na hatia ya kupokea rushwa ya zaidi ya yuan bilioni 2.2 (takribani dola za Marekani milioni 325 au zaidi ya shilingi bilioni 800 za Kitanzania) katika kipindi cha miaka 30 ya utumishi wake serikalini.
Mbali na kosa la rushwa, Yang mwenye umri wa miaka 69 alipatikana na hatia ya ubadhirifu wa mali za umma, matumizi mabaya ya madaraka pamoja na utakatishaji wa fedha.
Mahakama ilieleza kuwa,kiwango cha fedha alichojipatia kwa njia haramu ni miongoni mwa vikubwa zaidi kuwahi kurekodiwa nchini humo katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa mujibu wa uamuzi wa Mahakama ya Changzhou uliotolewa Jumatatu, Yang alitumia nyadhifa mbalimbali alizoshikilia katika Jiji la Nanjing kati ya mwaka 1993 na 2023 kuwasaidia wafanyabiashara na watu binafsi kupata zabuni za miradi ya ujenzi, uhamishaji wa ardhi na huduma za kifedha kwa kubadilishana na fedha taslimu na mali nyingine za thamani.
Mahakama ilibainisha kuwa,makosa hayo yalikuwa ya kiwango cha juu sana na yalisababisha hasara kubwa kwa maslahi ya taifa na wananchi wa China.
Yang alikuwa miongoni mwa viongozi waliochunguzwa chini ya kampeni kubwa ya kupambana na rushwa iliyoanzishwa na Rais wa China, Xi Jinping tangu alipoingia madarakani.
Kampeni hiyo imewahusisha maafisa waandamizi wa Serikali, viongozi wa sekta ya fedha, maafisa wa jeshi pamoja na taasisi nyingine za umma.
Ingawa kampeni hiyo imepongezwa kwa kuimarisha uwajibikaji katika utumishi wa umma, baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wamekuwa wakidai kuwa wakati mwingine hutumiwa pia kuwaondoa wapinzani wa kisiasa ndani ya chama tawala.
Adhabu ya kifo kwa makosa ya kifisadi nchini China hutolewa mara chache, lakini inaweza kutolewa pale ambapo kiwango cha rushwa kinachohusika ni kikubwa sana, hasa kinapozidi yuan bilioni moja.
Miongoni mwa kesi zinazofanana ni ile ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni ya Usimamizi wa Mali ya China Huarong, Lai Xiaomin ambaye alinyongwa mwaka 2021 baada ya kupatikana na hatia ya kupokea rushwa ya yuan bilioni 1.8 katika kipindi cha miaka 10.
Pia mwaka 2024, aliyekuwa ofisa wa Mkoa wa Inner Mongolia, Li Jianping alitekelezewa hukumu ya kifo baada ya kutiwa hatiani kwa ubadhirifu na rushwa iliyofikia zaidi ya yuan bilioni tatu.
Katika kesi nyingi zinazofanana, mahakama za China zimekuwa zikitoa adhabu ya kifo iliyosimamishwa, ambayo baadaye hubadilishwa kuwa kifungo cha maisha iwapo mfungwa ataonesha mwenendo mzuri gerezani.
Aidha, baadhi ya wahusika wamepunguziwa adhabu baada ya kushirikiana na mamlaka kufichua wahalifu wengine.
Hata hivyo, katika kesi ya Yang, mahakama ilisema kuwa licha ya kukiri makosa yake, kuonesha majuto na kushirikiana kwa kiwango fulani na vyombo vya uchunguzi, uzito wa makosa aliyoyatenda ulikuwa mkubwa kiasi kwamba haukustahili kupewa adhabu nafuu.
Yang alikiri makosa yote yaliyokuwa yanamkabili na kuomba msamaha mbele ya mahakama kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo.(NA)
