Kiswahili chaunganisha Tanzania na Oman, Ubalozi wa Tanzania waadhimisha kwa mara ya kwanza Siku ya Kiswahili Duniani jijini Muscat

MUSCAT-Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Oman umeadhimisha kwa mara ya kwanza Siku ya Kiswahili Duniani katika hafla maalum iliyofanyika katika Klabu ya Kidiplomasia (Diplomatic Club Oman) jijini Muscat.
Maadhimisho hayo yamefanyika miaka mitano tangu Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) litangaze rasmi tarehe 7 Julai kuwa Siku ya Kiswahili Duniani, hatua iliyothibitisha nafasi ya lugha hiyo kama nyenzo muhimu ya kuimarisha amani, mshikamano na mawasiliano ya kimataifa.

Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman Dkt. Mohammed Al Balushi alikuwa mgeni rasmi aliyeambatana na wawakilishi kutoka UNESCO, Chuo Kikuu cha Nizwa na Kituo cha Utamaduni cha Urusi, huku vyombo vya habari vya Muscat Daily, Oman Observer Daily, Gazeti la Kiarabu la Oman na Oman TV vikitoa uangalizi mkubwa wa tukio hilo.

Wananchi wa Oman pamoja na Watanzania wanaoishi nchini humo walijitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho hayo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Maulidah Hassan, alisema UNESCO kutangaza Julai 7 kama siku ya Kiswahili Duniani kulithibitisha umuhimu wa Kiswahili kama lugha ya amani, utambulisho na fahari inayozungumzwa na zaidi ya watu milioni 200 duniani.
Balozi Maulidah alisema kuwa Oman ina nafasi ya pekee katika historia ya Kiswahili kutokana na kuwa miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya wazungumzaji wa Kiswahili nje ya Bara la Afrika, ambapo kwa baadhi ya familia za Kiomani Kiswahili si lugha ya kigeni bali ni sehemu ya urithi wao wa kihistoria unaorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi.

Alieleza kuwa uhusiano wa Tanzania na Oman unaonekana katika maisha ya kila siku kupitia vyakula, mavazi na muziki na kutaja pilau, mandazi, chapati na maharage ya nazi kama vyakula vinavyounganisha jamii za pande zote za Bahari ya Hindi, huku baibui, kanzu na khanjar zikionesha mwingiliano wa muda mrefu wa tamaduni.

Alisema upepo wa Kaskazi na Kusi uliobeba majahazi ya kale haukusafirisha viungo na vitambaa pekee, bali pia familia, imani na urafiki, hivyo Tanzania na Oman zinapaswa kuendeleza urithi huo katika zama mpya kupitia diplomasia ya uchumi, utalii, usafirishaji, kilimo na uchumi wa buluu.
Maadhimisho hayo yalihitimishwa kwa burudani ya taarab, mapambo ya kitamaduni na vyakula vya asili vya Mswahili vilivyojumuisha mihogo ya nazi, maharagwe ya nazi, kisamvu na samaki.

Tukio hilo limeendelea kuonesha nafasi ya Kiswahili kama daraja la kuunganisha watu na mataifa, kuhifadhi urithi wa pamoja na kuimarisha uhusiano wa kihistoria, kiutamaduni na kidiplomasia kati ya Tanzania na Oman.

Hafla hiyo iliyobeba kaulimbiu “Kiswahili kwa Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Uchumi” ilihudhuriwa na mabalozi na wawakilishi zaidi ya 22 kutoka Nchi za bara la Ulaya, Amerika, Mashariki ya Kati, Bara Hindi na Afrika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here