NA DIRAMAKINI
MAKAMPUNI makubwa yanayozalisha saruji nchini Tanzania yameanza kutekeleza ongezeko la bei za bidhaa zao kuanzia mwanzoni mwa mwezi Julai,2026 hatua inayohusishwa na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji na uendeshaji wa biashara.
Makampuni yaliyotangaza marekebisho hayo ya bei ni pamoja na Dangote Cement, Moshi Cement (Jun Yu), Tanga Cement kupitia chapa ya Simba Cement, Lake Cement (Nyati Cement) na Mbeya Cement, ambapo yote yameeleza kuwa,mabadiliko hayo yamefanyika kutokana na sababu zinazofanana za kiuchumi zinazoathiri sekta ya uzalishaji.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na makampuni hayo, sababu kuu zilizochangia kupanda kwa bei ni kuongezeka kwa gharama za malighafi, gharama za uendeshaji wa biashara, ongezeko la tozo mbalimbali za kisheria na kodi, pamoja na kupanda kwa gharama za usafirishaji wa bidhaa kutoka viwandani hadi kwa wasambazaji na watumiaji.
Makampuni hayo yamebainisha kuwa marekebisho ya bei yaliyotangazwa hayajumuishi Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), hivyo bei halisi kwa mnunuzi itategemea utaratibu wa kodi unaotumika katika eneo husika.
Katika mabadiliko hayo, Dangote Cement imeongeza bei ya saruji kwa Shilingi 650 kwa kila mfuko wa kilo 50, huku Moshi Cement ikiongeza Shilingi 500 kwa kila mfuko kutoka bei iliyokuwa ikitumika awali.
Kwa upande wa Simba Cement inayozalishwa na Tanga Cement, kampuni hiyo imetangaza bei mpya ya Shilingi 13,000 kwa bidhaa husika, kiwango ambacho pia kimetangazwa na Lake Cement kupitia chapa yake ya Nyati Cement.
Mbeya Cement nayo imerekebisha bei za baadhi ya bidhaa zake, ambapo saruji ya FastaPlus imewekewa bei mpya ya Shilingi 9,085, huku Tembo Supaset ikitangazwa kwa Shilingi 14,136 kwa bidhaa husika.
Wadau wa sekta ya ujenzi wanaeleza kuwa, ongezeko hilo la bei linatarajiwa kuongeza gharama za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba, biashara na miundombinu, hasa kwa wakandarasi, wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi na wananchi wanaojenga kwa matumizi binafsi.
Hata hivyo, wachambuzi wa uchumi wanaeleza kuwa marekebisho ya bei katika sekta ya saruji mara nyingi hutokana na mabadiliko ya gharama za uzalishaji na usafirishaji, hivyo ni muhimu kwa wazalishaji na wadau wa sekta hiyo kuendelea kutafuta mbinu za kuongeza ufanisi ili kupunguza athari kwa watumiaji wa mwisho.
Ongezeko hilo linakuja wakati sekta ya ujenzi nchini inaendelea kukua kutokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali na sekta binafsi katika miradi ya miundombinu, makazi na viwanda, hali inayofanya saruji kuendelea kuwa miongoni mwa bidhaa muhimu katika shughuli za maendeleo ya uchumi.





