Mradi wa Dola milioni 110 wa ukaguzi wa kidijitali utapunguza ajali na rushwa barabarani-Kafulila

NA DIRAMAKINI

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), David Kafulila amesema,mradi wa dola za Marekani milioni 110 wa mfumo wa kidijitali wa ukaguzi wa usalama barabarani unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya usafiri kwa kupunguza ajali za barabarani, kuondoa usumbufu kwa madereva na kuongeza uwazi katika utekelezaji wa sheria za usalama barabarani.
Kafulila amesema,mfumo huo wa kisasa utatumia teknolojia za kidijitali kuboresha utendaji wa ukaguzi wa vyombo vya usafiri, huku ukipunguza utegemezi wa ukaguzi wa kawaida unaofanywa na binadamu, hatua ambayo itasaidia kuongeza ufanisi na uwajibikaji.

Ameeleza kuwa, pamoja na kubaini makosa mbalimbali ya usalama barabarani, mfumo huo utaweza kutambua makosa ya kibinadamu na kudhibiti mianya ya vitendo vya rushwa vinavyoweza kujitokeza wakati wa ukaguzi wa kawaida wa magari.

"Teknolojia hii itarahisisha utoaji wa huduma, kuongeza uwazi na kuhakikisha ukaguzi wa usalama barabarani unafanyika kwa ufanisi zaidi, huku ukipunguza nafasi ya makosa ya kibinadamu na vitendo vya rushwa,"amesema Kafulila.

Amebainisha kuwa,mradi huo ni mfano halisi wa namna ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi unavyoweza kutumika kuleta suluhisho bunifu kwa changamoto zinazowakabili wananchi, kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa na uwekezaji wa sekta binafsi.

Kafulila amesema,mfumo wa ubia wa PPP umeendelea kuwa nyenzo muhimu katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, kwani unaiwezesha Serikali kupata huduma na miundombinu ya kisasa bila kutegemea kikamilifu fedha kutoka Hazina.

Kwa mujibu wake, ushirikiano huo unaongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, huku ukiisaidia Serikali kuelekeza rasilimali zake katika maeneo mengine ya kipaumbele kama vile afya, elimu na huduma za jamii.

Aidha, amezitaka wizara, taasisi za Serikali na mashirika ya umma kufanya tathmini ya rasilimali walizonazo ambazo bado hazijatumika ipasavyo, ili ziweze kuingizwa katika miradi ya ubia na sekta binafsi kwa lengo la kuongeza thamani ya mali za umma na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Amesema, ipo fursa kubwa ya kutumia ardhi, majengo, miundombinu na rasilimali nyingine za Serikali kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi, hatua itakayochangia kuongeza mapato ya Serikali, kuimarisha utoaji wa huduma na kuzalisha ajira.

Kafulila amesisitiza kuwa,Serikali itaendelea kuhimiza matumizi ya mfumo wa PPP katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati, huku sekta binafsi ikishiriki kikamilifu katika safari ya maendeleo ya taifa.

Mradi huo wa ukaguzi wa kidijitali wa usalama barabarani unatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa inayotumia teknolojia katika kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara, kuongeza ufanisi wa usimamizi wa vyombo vya usafiri na kuimarisha uwazi katika utoaji wa huduma za umma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here