MBEYA-Mkuu wa Oparesheni Wilaya ya Kyela Mrakibu wa Polisi (SP) Misana Makweba kwa niaba ya Mkuu wa Polisi Wilayani humo Mrakibu wa Polisi (SP) Salehe Njama Julai 22, 2026 amewaongozwa Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa mama aitwaye Vaileth Peter aliyejifungua mapacha watatu wa kiume.
Akizungumza baada ya kutoa msaada huo kwa Mama huyo aliyepo katika Hospitali ya Wilaya ya Kyela, SP Makweba amesema kuwa msaada huo ni sehemu ya kuimarisha mahusiano na ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Jamii na ni sehemu ya kurejesha kwa jamii (Corporate Social Responsibility).
Aidha, SP Makweba amesema kuwa matendo hayo ya huruma ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Polisi kupitia Kamisheni ya Polisi Jamii yenye lengo la kuimarisha ushirikiano na mahusiano mazuri na wananchi, kufanya kazi karibu na jamii ili kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu katika jamii.
Kwa upande wake, Mama mzazi wa watoto hao Bi. Vaileth Peter amelishukuru Jeshi la Polisi Wilaya ya Kyela kwa kutoa msaada huo kwani utasaidia kukidhi mahitaji yake pamoja na watoto wake huku akisisitiza na kutoa wito kwa jamii kuunga mkono jitihada za Jeshi hilo katika kuzuia na kukabiliana na uhalifu.
Matendo hayo ya huruma yalienda sambamba na zoezi la usafi wa mazingira kuzunguka Hospitali hiyo pamoja na zoezi la utoaji wa damu salamu kwa wajili ya kuwasaidia wagonjwa mbalimbali wenye uhitaji ili kuokoa maisha yao.

