ARUSHA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Mawakili na Maafisa Sheria wa Serikali kuhakikisha sheria, mikataba na maamuzi ya Serikali vinalinda uhuru, usalama, rasilimali na maslahi ya Taifa.
Rais Dkt. Samia ametoa agizo hilo leo jijini Arusha wakati akifungua Mkutano Mkuu waMwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA).
Amesema ushindani wa kiuchumi na kisiasa duniani unaitaka Tanzania kuwa na mfumo imara wa sheria unaolinda mamlaka ya nchi, uchumi wake na rasilimali za Taifa.
Aidha, amewataka Mawakili wa Serikali kutambua vihatarishi vya kisheria mapema na kutoa ushauri kabla ya Serikali kuingia mikataba, kuanza miradi au kufanya maamuzi makubwa ili kuepusha hasara inayoweza kutokea kutokana na maamuzi hayo.
“Ni wajibu wenu kugundua vihatarishi mapema, kushauri kwa wakati na kuhakikisha nchi inalindwa kwa misingi imara ya kisheria,” amesema Rais Dkt. Samia.
Halikadhalika, amesisitiza ushirikishwaji wa Mawakili na Maafisa sheria katika hatua zote za maandalizi ya mikataba, manunuzi, uwekezaji, ardhi, ajira na miradi ya maendeleo.
Akizungumzia umuhimu na tija ya taaluma ya Sheria, Rais Dkt. Samia amesema Mwanasheria wa Serikali hapimwi kwa kesi alizoshinda pekee, bali pia kwa migogoro aliyoizuia, fedha za umma alizookoa na madhara aliyozuia kabla hayajatokea.
Rais Dkt. Samia pia ameonya dhidi ya matumizi yasiyofaa ya taaluma ya sheria ikiwemo kuhalalisha vitendo vinavyohatarisha amani, umoja, usalama na heshima ya Taifa.
“Tutasaidiwa kuiharibu nchi yetu, lakini hatutasaidiwa kuijenga tena. Tanzania ni yetu sote na tunapaswa kuilinda,”amesisitiza Rais Dkt. Samia.
Vilevile, ameziagiza taasisi za Serikali kuimarisha vitengo vya sheria na kuwajengea uwezo mawakili na maafisa sheria ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Ameongeza kuwa, utekelezaji wa Dira 2050 utahitaji usimamizi thabiti wa sheria, mikataba imara na taasisi zenye uwezo wa kulinda maslahi ya Taifa na wananchi kwa ujumla.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Zuberi Juma Homera, amesema Serikali imeendelea kupanua kanda za huduma za sheria kutoka moja hadi 11 ili kupeleka huduma karibu zaidi na wananchi na taasisi za umma nchini kote.
Amesema,Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imewafikia zaidi ya wananchi milioni nne nchi nzima na kusaidia kutatua migogoro mingi nje ya Mahakama.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Saidi Johari, amesema sheria zinapaswa kupimwa kwa matokeo yake katika uchumi, uwekezaji, huduma za jamii na maisha ya wananchi.
Amesema kitabu cha Falsafa ya Sheria ya Mama Samia kimeandaliwa ili kuweka kumbukumbu na ushahidi wa namna mageuzi ya sheria na sera yalivyochangia maendeleo ya nchi tangu mwaka 2021.
Naye, Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania, Bavoo Anatoly Junus amesema, mawakili wa Serikali wameokoa fedha nyingi za umma kupitia ushindi katika mashauri, usuluhishi wa migogoro na majadiliano yaliyozuia Serikali kuingia gharama kubwa.
Katika hafla hiyo pia, Rais Dkt. Samia ametunukiwa tuzo maalum kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria nchini.
Tags
Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania
Dr Samia Suluhu Hassan
Habari
Mkutano wa Mawakili wa Serikali
Mwanasheria Mkuu wa Serikali







