NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wateule kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, ushirikiano na bila upendeleo, wakitanguliza huduma kwa wananchi na maslahi ya Taifa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Ndugu Prisca Burton Lwangili kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwenye hafla iliyofanyika Ikulu ya Tunguu Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026.Rais Dkt. Samia ametoa maagizo hayo leo Ikulu, Tunguu, Zanzibar, baada ya kuwaapisha Naibu Makatibu Wakuu wawili na kushuhudia viongozi wengine wanne wakila Kiapo cha Uadilifu kwa Viongozi wa Umma.
Amesema uteuzi huo unaonesha imani ya Serikali kwa viongozi hao, akiwataka kutoa huduma bora katika kuwatumikia wananchi.
Rais Dkt. Samia pia ameiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais kuimarisha usimamizi wa masuala ya Muungano na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinatatuliwa kwa ushirikiano ili
kuendelea kuulinda na kuuimarisha Muungano.
Katika eneo la mazingira, amewataka viongozi kushirikiana kusimamia programu za uhifadhi na kukabiliana na changamoto zinazotishia mazingira na ustawi wa Taifa.
Aidha, ameitaka Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuimarisha usimamizi wa watumishi wa umma kwa kuweka mazingira yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Kwa sekta ya uchukuzi, Rais Dkt. Samia ameelekeza kuongezwa kasi katika ujenzi na usimamizi wa miradi ya reli, barabara, bandari na meli, pamoja na kutathmini namna ya kutanua biashara ya anga ya Shirika la Ndege la Tanzania.
Halikadhalika, ameitaka Wizara ya Katiba na Sheria kuendelea kuimarisha upatikanaji wa haki nchini, na kuzipa msukumo kampeni za msaada wa kisheria ili huduma za kisheria ziwafikie wananchi kwa waingi na kuwasaidia kupata haki zao kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ameitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuimarisha ukuzaji wa biashara na usimamizi wa maonesho ya biashara nchini.
Vilevile, ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuimarisha usimamizi
na ulinzi wa hifadhi za wanyamapori pamoja na rasilimali za utalii, akisisitiza kuwa taasisi
hiyo ina nafasi muhimu katika kulinda na kukuza sekta ya utalii nchini.
Kwa upande wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Rais Dkt. Samia amelitaka shirika hilo kuimarisha nafasi yake kama chombo cha Serikali na sauti ya Taifa, kwa kukuza ubora wa maudhui, pamoja na ufanisi na weledi wa watumishi wake.
Walioapishwa ni Dkt. Latifa Mohammed Khamis, aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano, na Bi. Prisca Burton Lwangili, aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Viongozi Wateule wakiapa kiapo cha uadilifu kwa Viongozi wa Umma kwenye hafla iliyofanyika Ikulu ya Tunguu Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026.Viongozi wengine walioapa Kiapo cha Uadilifu kwa Viongozi wa Umma ni Bw. Ephraim Mafuru, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE); Bw. Salum Nassor Mnuna, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA); Bw. Massana Gibril Mwishawa, Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Bi.Asha Dachi Mbaruk, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
