NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anaondoka nchini leo tarehe 31 Julai, 2026 kwenda nchini Angola kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Angola, Mheshimiwa João Manuel Gonçalves Lourenço.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu,Bakari S.Machumu.Akiwa nchini humo, Rais Dkt. Samia na mwenyeji wake, Rais Lourenço, watashiriki katika hafla ya uzinduzi wa hospitali ya rufaa iliyopewa jina la Baba wa Taifa,Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, iliyopo jijini Luanda. Hafla hiyo pia itahudhuria na familia ya Baba wa Taifa ikiongozwa na Mama Maria Nyerere.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mama Maria Nyerere muda mfupi kabla ya kuanza safari ya kuelekea Luanda, Angola ambapo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya Uzinduzi wa Hospitali iliyopewa jina la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, tarehe 31 Julai, 2026.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiagana na viongozi mbalimbali kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam kabla ya kuondoka nchini, kuelekea Luanda, Angola ambapo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya Uzinduzi wa Hospitali iliyopewa jina la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, tarehe 31 Julai,2026.
Aidha, Rais Dkt. Samia atafanya mazungumzo na Rais Lourenço na kushiriki hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Wake wa Marais wa Afrika kwa lengo la kuchangisha fedha za utekelezaji wa shughuli za kijamii na kiuchumi za uwezeshaji wa wanawake na vijana.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa kuimarisha uhusiano wa kihistoria na wa kindugu kati ya Tanzania na Angola, uliojengwa tangu enzi za harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.




