DAR-Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUTSO), Ndg. Felix Lugeiyamu, amekipongeza Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwa kuendelea kuwajali wanafunzi kupitia uanzishaji wa programu mpya za masomo zinazokidhi mahitaji ya sasa ya soko la ajira na kupanua wigo wa uchaguzi wa taaluma kwa waombaji wa elimu ya juu.
Akizungumza baada ya kutembelea banda la OUT katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), Ndg. Lugeiyamu alisema hatua ya kuanzishwa kwa programu mpya, hususan katika ngazi ya shahada ya kwanza, inaonesha dhamira ya chuo ya kuendelea kutoa elimu yenye ubora, inayoendana na mahitaji ya taifa na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, alieleza kuridhishwa na ubora wa huduma zinazotolewa katika banda la OUT, akibainisha kuwa wageni wanapata huduma kwa haraka kupitia ushauri wa kitaalamu, udahili wa papo kwa papo, pamoja na ufafanuzi wa kina kuhusu programu mbalimbali za masomo na huduma nyingine za chuo.
Katika hatua nyingine, Ndg. Lugeiyamu aliwahamasisha walimu wenye Stashahada ya Ualimu wa Shule za Msingi kuchangamkia fursa ya kujiunga na programu mpya ya Shahada Jumuishi ya Umahiri katika Elimu ya Ualimu wa Shule za Msingi, akieleza kuwa programu hiyo imebuniwa mahsusi kuwapa walimu nafasi ya kujiendeleza kitaaluma kwa mfumo unaowapa unafuu wa kusoma huku wakiendelea kutekeleza majukumu yao ya kazi.
Alisema programu hiyo humwezesha mwanafunzi kuhitimu ndani ya kipindi cha miaka 3 hadi 6, kulingana na ratiba na majukumu yake binafsi na ya kikazi.Vilevile, inawawezesha walimu kuendelea na safari yao ya kitaaluma kutoka Shahada ya Kwanza hadi Shahada ya Uzamili kupitia mkondo mmoja jumuishi.
"Ninawahimiza wananchi wote wanaotamani kujiunga na OUT kutembelea banda letu katika Maonesho ya Sabasaba ili kupata maelezo ya kina kuhusu programu hizi mpya na nyingine zinazotolewa na chuo.
Pia watapata fursa ya kusaidiwa papo kwa papo endapo watakuwa na changamoto zinazohusu udahili, usajili au huduma nyingine za kitaaluma," alisema.
OUT inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya kupanua fursa za elimu kupitia programu bunifu, matumizi ya teknolojia na utoaji wa huduma bora zinazowawezesha Watanzania wengi zaidi kufikia ndoto zao za elimu bila kuathiri majukumu yao ya kila siku.

