■Tanzania yajipanga kuwa kitovu cha huduma bora za maabara ya madini Kusini mwa Jangwa la Sahara
DODOMA-Kufuatia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa maabara ya kisasa ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), hatua hiyo inakwenda kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utoaji wa huduma za maabara ya madini kusini mwa Jangwa la Sahara.
Hayo yamesemwa leo Julai 15,2026 na Waziri wa Madini,Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb) alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa maabara ya GST uliopo Kizota jijini Dodoma.
"Tunamshukuru Rais wetu Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huu wa kisasa, unaokwenda kuifanya Nchi yetu kuwa kinara na mahiri katika utoaji wa huduma za maabara za madini.
"Mradi huu pia unakwenda kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utoaji wa huduma za maabara kwa Nchi za Afrika ya Mashariki na Kati, kutokana na ubora wa huduma hizo kuwa za kimataifa,"ameeleza Waziri Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde amebainisha kuwa,kwa muda mrefu wachimbaji wadogo wamekuwa wakipata changamoto ya upimaji wa sampuli zao kwenye maabara, hali iliyopelekea kushindwa kufanya shughuli zao kiufanisi.
Mavunde alisisitiza kuwa,ujio wa maabara hiyo ya kisasa unakwenda kuwa mwarobaini wa changamoto za wachimbaji ikiwa ni pamoja na kuhudumia wachimbaji wengi zaidi kwa ubora wa kimataifa.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Madini Tanzania, Mhandisi Ally Samaje ameeleza kuwa,ujenzi wa mradi huo wa maabara unagharimu shilingi bilioni 14.3 na upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambapo unatarajia kukamilika ifikapo Septemba, 2027.
Aidha,ameongeza kuwa maabara hiyo ikikamilika itakuwa ni ya kisasa na inakwenda kuhudumia wateja wengi wa ndani na nje ya nchi.
Tags
Anthony Mavunde
Habari
Maabara ya Madini Dodoma
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST)
Wizara ya Madini Tanzania














