NA MUNIR SHEMWETA,
New York
TANZANIA imeeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utekelezaji wa Ajenda Mpya ya Miji (New Urban Agenda) katika kipindi cha miaka 10, ikiwemo kupungua kwa umaskini wa upatikanaji wa huduma za msingi, kuongezeka kwa umiliki wa ardhi kwa wanawake na kurasimishwa kwa zaidi ya milki milioni 1.1 za ardhi.
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa-New York Mhe. Balozi Togolani Mavura (kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga (Katikati) na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Bw. Deogratius Kalimenze wakiwa katika mkutano wa ngazi ya juu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Makazi (UN Habitat) kuhusu mapitio ya utekelezaji wa ajenda mpya ya miji kwa kipindi cha miaka 10 tarehe 16 Julai 2026.Mafanikio hayo yamewasilishwa katika tamko la Tanzania kwenye Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Makazi (UN-Habitat) kuhusu mapitio ya utekelezaji wa Ajenda Mpya ya Miji kwa kipindi cha miaka 10, unaofanyika Julai 16 hadi 17, 2026 katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Togalani Mavura. Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bw. Sospeter Mtwale pia wanashiriki mkutano huo.
Katika tamko hilo, Tanzania ilieleza kuwa kiwango cha umaskini wa upatikanaji wa huduma za msingi (Basic Needs Poverty) kimepungua kutoka asilimia 36 mwaka 2000 hadi asilimia 26 mwaka 2024, hatua inayotajwa kuwa matokeo ya juhudi za serikali katika kuboresha maisha ya wananchi.
Vilevile, serikali imeendelea kuboresha makazi holela kwa kurasimisha zaidi ya milki milioni 1.1 za ardhi, huku umiliki wa ardhi kwa wanawake ukiongezeka kutoka asilimia 28 hadi asilimia 37.4 mwaka 2024.
Tanzania pia imeeleza kuwa imeendelea kupanua upatikanaji wa mikopo ya nyumba kupitia Tanzania Mortgage Refinance Company (TMRC), hatua iliyochangia kupungua kwa viwango vya riba ya mikopo ya nyumba hadi kati ya asilimia 15 na 19 ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kumudu kumiliki nyumba.
Aidha, serikali imefanya mapinduzi makubwa katika upatikanaji wa huduma za msingi, miundombinu na matumizi ya Tehama katika utoaji huduma mbalimbali pamoja na maboresho makubwa katika sekta ya ardhi.
Mkutano huo wa siku mbili unajadili utekelezaji wa Ajenda Mpya ya Miji tangu ilipopitishwa mwaka 2016, pamoja na kuweka mikakati ya kuharakisha utekelezaji wake katika kipindi kilichosalia.
Ajenda Mpya ya Miji ni mpango wa kimataifa wa miaka 20 uliopitishwa Oktoba 2016 katika Mkutano wa Habitat III uliofanyika Quito, Ecuador.
Sehemu ya washiriki wa mkutano wa ngazi ya juu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Makazi (UN Habitat) unaopitia utekelezaji wa ajenda mpya ya miji kwa kipindi cha miaka 10. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI).
Sehemu ya washiriki wa mkutano wa ngazi ya juu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Makazi (UN Habitat) unaopitia utekelezaji wa ajenda mpya ya miji kwa kipindi cha miaka 10. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI).Ajenda hiyo inalenga kutoa dira ya kimataifa ya upangaji, uendelezaji na usimamizi miji kwa kuhimiza ukuaji wa miji unaozingatia usawa wa kijamii, ustawi wa kiuchumi, ulinzi wa mazingira, upatikanaji wa makazi salama na huduma bora za msingi, sambamba na kuchangia utekelezaji wa Lengo la 11 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) la kujenga miji jumuishi, salama, himilivu na endelevu.
