KIGOMA-Shirika la Reli Tanzania (TRC) limekamilisha zoezi la ulipaji wa fidia ya km 72 za njia kuu na vipande vya ardhi vya km 44 kwa wananchi waliotwaliwa maeneo yao kupisha ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha sita Tabora–Kigoma, lililoanza tarehe 15 Julai 2026.
Katika zoezi hilo, jumla ya shilingi 6,537,400,478.50 zimelipwa kwa wanufaika 1,552 kutoka Halmashauri za Wilaya za Kigoma, Uvinza, Urambo, Kaliua na Uyui pamoja na Manispaa ya Tabora, ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya Ardhi na Sheria ya Utwaaji Ardhi.
Fidia hiyo ilihusisha maeneo yaliyotwaliwa kwa ajili ya ujenzi kambi (campsites), njia kuu ya reli, maeneo ya kuchimba na kutupa kifusi, njia za ziada (access roads) pamoja na maeneo ya kuchimba mchanga.
Sambamba na ulipaji wa fidia, TRC iliendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi bora ya fedha za fidia, ikiwahimiza kuzielekeza katika shughuli za maendeleo na uwekezaji wenye tija kwa familia na jamii.
Kukamilika kwa zoezi hilo kunafungua hatua inayofuata ya utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa SGR kipande cha sita Tabora–Kigoma, huku TRC ikiendelea kushirikiana na wananchi na wadau kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia taratibu zote za kisheria.
