TANGA-Wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kwamsisi, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wamehimizwa kutekeleza wajibu wao wa kufuatilia na kusimamia maendeleo ya watoto wao kwa kushirikiana na walimu ili kuongeza ufaulu shuleni.
Wito huo ulitolewa Julai 15, 2026 na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mkata, SP Juma R. Wandi, wakati wa kikao cha wazazi na wanafunzi wa shule hiyo kilichohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa eneo hilo.
SP Wandi aliwataka wazazi kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia na kuhimiza matumizi ya hosteli ili kuongeza muda wa masomo. Pia aliwataka wanafunzi kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kuathiri elimu yao.
Aidha, alichangia shilingi 30,000 kwa ajili ya gunia moja la mahindi na kutoa zawadi kwa wanafunzi watano waliofanya vizuri katika mtihani wa Mock.
Wazazi na uongozi wa shule walilishukuru Jeshi la Polisi kwa elimu na hamasa iliyotolewa, huku wakiahidi kuendelea kushirikiana katika kuboresha ufaulu wa wanafunzi.

