DAR-Wananchi na viongozi mbalimbali waliotembelea Banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika Maonesho ya 60 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, wamenufaika na elimu ya majukumu ya BoT pamoja na elimu ya masuala mbalimbali ya fedha.
Bi. Zainab Mtweve kutoka Morogoro ni miongoni mwa waliotembelea banda hilo na amesema elimu kuhusu utunzaji wa akiba, mikopo na uwekezaji katika dhamana za serikali itamsaidia katika utunzaji wa akiba itamsaidia kusimamia fedha zake kwa ufanisi na uwekezaji wa baadae.
Kwa upande wake, Bw. Ahmed Wazir Mohamed mkazi wa Bunju jijini Dar es salaam, amesema kwa kutembelea banda hilo amepata elimu ya namna Benki Kuu inadhibiti mfumuko wa bei kwa kutumia Sera ya fedha kwa ajili ya kustawisha uchumi wa nchi
Pia, kupitia maonesho haya, BoT inaelimisha umma kuhusu majukumu mengine amabayo ni pamoja na kutoa sarafu ya nchi ambayo ni Shilingi ya Tanzania, kusimamia na kudhibiti mabenki na taasisi za fedha, kusimamia na kudhibiti mifumo ya malipo nchini na kuhifadhi akiba ya nchi ikiwemo fedha za kigeni.
Vilevile, wananchi wanaelezwa kuhusu utaratibu wa kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za kifedha masuala ya ajira na utumishi ndani ya Benki Kuu, pamoja na fursa za masomo zinazotolewa na Chuo cha BoT.
Maonesho hayo, yenye kaulimbiu isemayo, "Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba, Fahari ya Tanzania," yalianza Juni 28, 2026 na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 13, 2026.









