ARUSHA-mmoja amefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa kufuatia ajali ya basi kugongana na gari ndogo huko katika barabara ya Arusha- Moshi maeneo ya King’ori, wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Akitoa taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo amesema ajali hiyo imetokea Agosti 08 mwaka huu, muda wa saa 04:30 asubuhi na kueleza kuwa baada ya kugongana magari hayo yaliwaka moto na kupelekea kifo kwa abiria mmoja raia wa kigeni na majeruhi wawili waliokuwa kwenye gari ndogo.
Amebainisha kuwa ajali hiyo ilihusisha basi lenye namba za usajili T. 639 AQN, aina ya Scania lililokuwa linatokea Arusha kuelekea Mkoani Tanga kugongana na gari ndogo aina ya Alphard lenye namba za usajili T. 837 EMS lililokuwa linatokea Kilimanjaro kuelekea mkoani Arusha.
Aidha, Kamanda Masejo amesema wanaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limetoa wito kwa madereva kuhakikisha wanazingatia na kufuata sheria za usalama barabarani huku likisema litaendelea kuchukua hatua kwa watakaobainika kukiuka sheria hizo.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Arusha, SSF Osward Mwanjejele amesema mara baada kupokea taarifa hiyo, walifika mara moja na kufanikiwa kuokoa abiria wote waliokuwa kwenye basi na majeruhi wawili waliokuwa kwenye gari ndogo huku pia wakifanikiwa kuzima moto huo.

