NA DIRAMAKINI
RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne,Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema,Afrika inapaswa kuondoka katika mtazamo wa kupima maendeleo kwa idadi ya barabara, bandari au mitambo ya kuzalisha umeme pekee, na badala yake kuelekeza nguvu katika kujenga miundombinu itakayowawezesha vijana kupata elimu, ujuzi, ajira na uwezo wa kushindana katika uchumi wa dunia unaobadilika kwa kasi.
Dkt.Kikwete ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam aliposhiriki mjadala uliohusu "Miundombinu: Chachu ya Ukuaji wa Uchumi na Msingi wa Nguvu Kazi ya Baadaye ya Afrika", uliofanyika sambamba na Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 pamoja na Jukwaa la Miundombinu Afrika.
Amesema,mafanikio ya miradi ya maendeleo hayapaswi kupimwa kwa ukubwa au idadi ya miundombinu inayojengwa pekee, bali kwa kiwango ambacho imechangia kuboresha maisha ya wananchi kupitia kuongeza ajira, kuchochea biashara, kuvutia uwekezaji na kuinua ustawi wa jamii.
Dkt.Kikwete amesema,Afrika inapaswa kujiuliza kama miundombinu inayojengwa leo inaendana na mahitaji ya uchumi wa siku zijazo, akieleza kuwa ifikapo mwaka 2030 zaidi ya vijana milioni 12 wataingia katika soko la ajira kila mwaka, huku ifikapo mwaka 2050 bara hilo likitarajiwa kuwa na zaidi ya robo ya watu wote wenye umri wa kufanya kazi duniani.
Pia, amesema ongezeko hilo la vijana linaweza kuwa mtaji mkubwa wa maendeleo ikiwa wataandaliwa kupitia elimu bora, mafunzo ya ujuzi na fursa za ajira zinazokidhi mahitaji ya uchumi wa kisasa.
"Hata hivyo,bila maandalizi ya kutosha, ongezeko hilo linaweza kuongeza changamoto za ukosefu wa ajira, umaskini, kukata tamaa kwa vijana na kuhatarisha utulivu wa kijamii."
Rais huyo mstaafu amesisitiza kuwa,uwekezaji katika elimu unapaswa kwenda sambamba na uwekezaji katika miundombinu ili kuzalisha nguvu kazi yenye maarifa, ubunifu na uwezo wa kushindana katika soko la ajira la kimataifa.
Akizungumzia mapinduzi ya teknolojia duniani, Dkt.Kikwete amesema,dunia tayari imeingia katika enzi ya matumizi ya Akili Unde (AI), hivyo Afrika haina budi kuwaandaa vijana wake si kwa ajili ya kutumia teknolojia hiyo pekee, bali pia kuibuni, kuiboresha na kuitumia kama msingi wa kuanzisha biashara na viwanda vipya.
Amesema, bara la Afrika halipaswi kubaki kuwa soko la teknolojia zinazotengenezwa nje ya bara, bali linapaswa kushiriki kikamilifu katika utafiti, ubunifu, uhandisi na maendeleo ya teknolojia ili kuongeza ushindani wake duniani.
Aidha, Dkt. Kikwete amesema,maandalizi ya nguvu kazi ya baadaye yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya serikali na sekta binafsi, ambapo serikali zinapaswa kuweka sera rafiki, kuimarisha mifumo ya elimu na kuwekeza katika miundombinu muhimu, huku sekta binafsi ikichukua nafasi kubwa katika kuwaandaa vijana kwa ujuzi unaohitajika katika uchumi wa kisasa.
Naye Rais wa kampuni ya kimataifa ya teknolojia ya mPedigree, Bright Simmons amesema,Afrika inapaswa kutambua tofauti kati ya teknolojia zinazoweza kutumika bila kubadili mfumo wa uchumi na zile zinazohitaji mageuzi makubwa ya kiuchumi ili kuleta manufaa ya kweli.
Simmons amesema,Akili Unde inaweza kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo endapo itaambatana na uwekezaji katika miundombinu, elimu,ujuzi wa watu na mageuzi ya mifumo ya uzalishaji.
Ameongeza kuwa,Afrika ina hazina kubwa ya vipaji na maarifa ambayo bado hayajatumika kikamilifu, hasa miongoni mwa vijana wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi kama kilimo, utengenezaji wa bidhaa na shughuli nyingine za uzalishaji.
Amesisitiza kuwa, kuwapa vijana hao teknolojia, mafunzo na fursa za maendeleo kutasaidia kuongeza tija, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuharakisha safari ya bara hilo kuelekea mapinduzi ya viwanda na maendeleo endelevu.




