NA DIRAMAKINI
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limemkamata na linaendelea kumhoji mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Elizabeth Chacha Mgushi, miaka 30 ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa mtaa wa Ziwa, Kata ya Butimba, Wilaya ya Nyamagana kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuwa ametekwa.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa.
Ameeleza kwamba, mnamo tarehe 25 Julai, 2026 majira ya saa 8:45 usiku, katika mtaa wa Ziwa, Kata ya Butimba, mwanamke huyo bila huruma aliwaacha watoto wake wanne wenye umri mdogo wakiwa wamelala akiwemo mtoto wa miaka 2 bila uangalizi wa mtu yeyote na kuwatoroka kwenda mkoa wa Singida kuonana na mchepuko wake.
Mtuhumiwa huyo, akiwa njiani kuelekea Singida alitoa taarifa za uongo kwa mume wake aliyebahatika kupata naye watoto hao pamoja na ndugu zake akidai kuwa ametekwa na watu asiowafahamu na kwamba watekaji hao walikuwa wakitaka walipwe kiasi cha fedha cha shilingi 800,000 ili waweze kumwachia huru.
Baada ya taarifa hizo kuripotiwa katika kituo cha Polisi, uchunguzi na ufuatiliaji wa kiina ulianza maramoja na ilipofika tarehe 26 Julai, 2026, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kumtia mbaroni mwanamke huyo akiwa salama mwenye afya njema.
Katika mahojiano ya awali, mtuhumiwa amedai kuwa alisukumwa na ugumu wa maisha ya ndoa kutokana na kutingwa kwa majukumu kwa mume wake ambaye husafiri mikoani kufanya biashara ya kuuza vyombo vya ndani na alikuwa hajarejea nyumbani kwa takribani miezi minne.
Chanzo cha tukio hili ni tamaa za mahusiano ya kimapenzi. Mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi na taratibu za kisheria zinaendelea ili afikishwe mahakamani kujibu tuhuma za kutoa tarifa za uongo.
Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wananchi wote kuacha tabia ya kutoa taarifa za uongo au kujitungia matukio yanayozua taharuki kama kujiteka kwa nia ya kujipatia fedha, kufanya mzaha au kutatua changamoto za kifamilia.
Kitendo hiki ni kosa kisheria na kinapoteza rasilimali na muda mwingi wa Jeshi la Polisi ambao ungetumika kuzuia na kuchunguza uhalifu wa kweli.
Vilevile, Jeshi la polisi linahimiza familia na wanandoa kutatua migogoro au changamoto za kifamilia kwa njia za amani, ushauri nasaha au kupitia vyombo vinavyotambulika kisheria.
