Hersi Said ateuliwa tena urais wa Yanga SC kwa miaka minne

NA DIRAMAKINI

WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Klabu ya Yanga wamempa kura ya kuendelea kuiongoza klabu hiyo Rais Hersi Said, baada ya kumthibitisha kwa kishindo kuendelea kushika nafasi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka minne.
Hersi amethibitishwa katika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi uliofanyika leo Agosti 2,2026 katika Ukumbi wa The Super Dome uliopo Masaki, Dar es Salaam, ambapo wajumbe pia wamemthibitisha Arafat Haji kuendelea kuwa Makamu wa Rais wa klabu hiyo kwa kipindi kingine cha miaka minne.

Mwenyekiti wa Uchaguzi wa Yanga, Malangwe Mchungahela, amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya wanachama kuridhia kwa kauli moja majina ya viongozi hao kuendelea kuongoza klabu.

Akizungumza katika mkutano huo, Mchungahela ametangaza rasmi ushindi wa Hersi na Arafat, akisema mchakato huo umefanyika kwa kuzingatia masharti ya Katiba ya klabu.

“Kwa mujibu wa Ibara ya 23(3) na 24(1), nawatangaza rasmi Hersi na Arafat kushika nyadhifa za Urais na Makamu wa Urais,” amesema Mchungahela.
Matokeo hayo yanawapa Hersi Said na Arafat Haji dhamana ya kuendelea kusimamia uendeshaji na maendeleo ya Yanga kwa kipindi kingine cha miaka minne.

Kuthibitishwa kwa viongozi hao kunaashiria mwendelezo wa uongozi wa klabu hiyo, huku wanachama wakitarajiwa kuendelea kutazama utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya klabu katika kipindi kipya cha uongozi.

Uongozi huo mpya utakuwa na jukumu la kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi kilichopita, sambamba na kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika uendeshaji wa klabu, ushindani wa ndani na wa kimataifa, pamoja na kuimarisha maslahi ya wanachama na taasisi ya Yanga kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here