■Bei zitaendelea kuwa za kawaida na rafiki kwa wateja
DAR-Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, imesema wafanyabiashara hao wana uzoefu na weledi mkubwa wa kuhudumia wateja wa ndani na wa kimataifa, hivyo wako tayari kuwahudumia wageni watakaokuja nchini wakati wa AFCON2027.
Hayo yamesemwa leo na Msemaji wa Jumuiya hiyo Hendry Kanje kuwa, wafanyabiashara hao wamekuwa wakifanya biashara na watu kutoka mataifa mbalimbali na kusafiri mara kwa mara katika nchi kama Uturuki, China, Japan, Malaysia na Dubai kufuata bidhaa.
“Tuna wafanyabiashara wanaojua lugha mbalimbali, ikiwamo Kiingereza, Kifaransa na Kichina, hivyo tuna uwezo wa kuwasiliana na kuwahudumia wageni kutoka mataifa mbalimbali,” amesema.
Amesema Jumuiya imejipanga kuhakikisha Kariakoo inatoa huduma kwa weledi, kuzingatia huduma bora kwa wateja na usalama wa wageni wakati wote wa mashindano hayo.
Aidha, amesema bei za bidhaa zitaendelea kuwa za kawaida na rafiki kwa wateja, kwa kuwa wafanyabiashara wanazingatia kuongeza mzunguko wa biashara kwa kupata faida inayowawezesha kuendelea kuagiza bidhaa nyingine.
Kanje amesema AFCON2027 pia itakuwa fursa ya kuunganisha wafanyabiashara wa Kariakoo na wafanyabiashara kutoka mataifa yatakayoshiriki mashindano hayo.
“Kariakoo ina bidhaa nyingi zinazotengenezwa ndani na nje ya nchi, hivyo tunataka AFCON2027 itumike pia kufungua fursa mpya za biashara na kukuza mahusiano ya kibiashara na mataifa mbalimbali,” amesema.

