DAR-Mfanyabiashara na Msemaji wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Bw. Hendry Kanje, amesema wafanyabiashara wa Kariakoo wana matumaini makubwa na michuano ya AFCON2027 huku wakiiombea timu ya Taifa, Taifa Stars, kufanya vizuri na hatimaye kutwaa ubingwa huo na kulibakiza kombe nchini Tanzania.
Kanje amesema moja ya urithi mkubwa wanaoutamani kuuona kupitia AFCON2027 ni Tanzania kufanya vizuri katika mashindano hayo na Taifa Stars kuibuka mabingwa, jambo ambalo kwa maoni yake litaipa Tanzania nafasi kubwa zaidi katika ramani ya soka na dunia kwa ujumla.
“Kwanza tunaiombea timu yetu ya Taifa ishinde na kuchukua kombe la AFCON2027. Pili, urithi mwingine ni kwamba klabu kubwa za soka Tanzania zipo hapa Kariakoo, Jangwani na Msimbazi. Fedha zitakazotumika kununua bidhaa Kariakoo wakati wa AFCON2027 ni jambo ambalo tutalikumbuka sana,” amesema Kanje.
Aidha, Kanje amesema wafanyabiashara wa Kariakoo wako tayari kuendeleza utamaduni wao wa ukarimu kwa wageni watakaofika nchini kwa ajili ya michuano hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wageni wanapata huduma bora katika maeneo mbalimbali ya soko hilo.
“Tunataka wageni watakapotoka Kariakoo waone kwamba hili ni soko la kimataifa, na wasitembee eneo moja tu bali watembelee maeneo mbalimbali ya soko letu. Tunawaomba wafanyabiashara wenzetu wajipange vizuri kuwahudumia wageni na kuendeleza ukaribu ambao umekuwa sehemu ya utamaduni wetu, kwa sababu kufanya hivyo ni kupeleka sifa njema ya Tanzania kwa mataifa mengine,” amesema Kanje.
Kwa mujibu wa Kanje, AFCON2027 pia itakuwa fursa muhimu kwa wafanyabiashara wa Kariakoo kunufaika kiuchumi kutokana na ongezeko la wageni, mashabiki wa soka na matumizi yatakayofanyika nchini katika kipindi cha mashindano.
Amesema wafanyabiashara wanapaswa kutumia fursa hiyo kwa kujiandaa mapema, kuhakikisha huduma zao zinaendana na hadhi ya soko la kimataifa na kuendelea kudumisha ukarimu ambao umekuwa sehemu ya utambulisho wa Kariakoo.
Kanje ameongeza kuwa, mafanikio ya AFCON2027 hayatapimwa kwa upande wa michezo pekee, bali pia kwa namna Tanzania itakavyotumia mashindano hayo kutangaza utamaduni, biashara na fursa mbalimbali zilizopo nchini
