Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mlima Kilimanjaro (MK-ICC) jijini Arusha kuhudumia watu 5000 kwa wakati mmoja-Waziri Kombo

DODOMA-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb), amesema kuwa, ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mlima Kilimanjaro (MK-ICC) jijini Arusha, utaongeza uwezo wa Tanzania katika kuandaa mikutano ya kitaifa, kikanda na kimataifa kwa kuondoa changamoto ya muda mrefu ya nchi ya kutokuwa na kumbi za kubeba watu wengi kwa wakati mmoja.
Waziri Kombo ametoa kauli hiyo wakati wa kikao kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) chini ya mwenyekiti wake, Mhe. Najma Murtaza Giga (Mb) na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kilichofanyika kwenye ukumbi wa Bunge jijini Dodoma Agosti 12, 2026.

Balozi Kombo alieleza kuwa ujenzi huo ni utekelezaji wa vitendo wa Diplomasia ya Uchumi kupitia utalii wa mikutano; kuvutia uwekezaji wa ndani na nje; kuongeza ajira; kuvutia utalii; kuongeza mapato ya Serikali; kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kuchochea maendeleo ya sekta za utalii, biashara, huduma na usafiri.
Kituo hicho kinachojengwa kwa ushirikiano kati ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) kinahusisha ujenzi wa ukumbi wa mikutano wa kisasa unaijumuisha, ukumbi mkuu wa mikutano wenye uwezo wa kuhudumia washiriki 5,000; kumbi ndogo za mikutano zenye uwezo wa kuhudumia washiriki kati ya 30 hadi 500; ukumbi wa hadhi ya Viongozi Wakuu wa Kitaifa wenye uwezo wa kuhudumia watu 300, ukumbi wa maonesho wenye eneo la uwezo wa kuhudumia washiriki 10,000 na jengo la utawala.
Vilevile kutakuwa na hoteli ya nyota tano yenye vyumba 500; eneo la maegesho ya magari yenye uwezo wa kuhudumia magari 2,000; pamoja na miundombinu yote ya nje inayohitajika kwa uendeshaji wa Kituo hicho yenye jumla ya ukubwa wa mita za mraba 50,000.

Kwa upande wao wajumbe wa Kamati ya NUU walipongeza ujenzi huo na kubainisha kuwa utakapokamilika utakuwa alama kwa Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Aidha, waliitaka Wizara kupitia AICC kujipanga vyema ili kituo hicho kiweze kutoa huduma bora na kukifanya kuwa shindani duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here