NA DIRAMAKINI
RAIS wa Msumbiji, Mheshimiwa Daniel Chapo ametangaza kuanzishwa kwa mpango mpya wa Pró-Jovem unaolenga kuchukua nafasi ya Mfuko wa Kusaidia Mipango ya Vijana (FAIJ) na kupanua fursa za upatikanaji wa fedha kwa miradi ya vijana katika wilaya zote nchini humo.
Msumbiji imegawanywa katika mikoa 10 na Jiji moja lenye hadhi ya mkoa la Maputo, na mikoa hiyo imegawanywa zaidi katika wilaya zaidi ya 140 kwa ujumla.
Ametangaza mpango huo jana mjini Pemba, Mkoa wa Cabo Delgado wakati akifungua Mkutano wa Tisa wa Kitaifa wa Vijana, uliobeba kaulimbiu “Vijana, Kesho ni Sasa!” ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani humo.
Mheshimiwa Chapo amesema,uamuzi wa kuanzisha Pró-Jovem umefikiwa baada ya Serikali kufanya tathmini ya utekelezaji wa FAIJ na kubaini changamoto mbalimbali ikiwemo ucheleweshaji wa utoaji wa fedha, ufuatiliaji usiotosheleza wa miradi, ugumu wa kupata fedha,urasimu pamoja na ukomo wa bajeti.
“Tunatangaza kuanzishwa kwa mpango madhubuti wa kusaidia miradi ya vijana,” amesema Rais Chapo akieleza kuwa,mfumo huo mpya utalenga kuhakikisha vijana katika wilaya zote wanapata fursa pana zaidi za kupata mitaji ya kutekeleza miradi yao.
Rais Chapo amesema, Pró-Jovem unatarajiwa kuendeshwa kwa mfumo unaofanana na Mpango wa Ustahimilivu na Fursa kwa Wanawake (PRO-MULHER) pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Uchumi wa Mitaa (FDEL) jambo litakalowezesha mpango huo kuwafikia vijana katika maeneo mengi zaidi ya nchi.
Wakati huo huo,Rais Chapo ametangaza kuwa Serikali itaongeza mara mbili, baadaye mwaka huu thamani ya mkataba wa mpango uliosainiwa kati ya Serikali na Baraza la Taifa la Vijana (CNJ) kwa ajili ya kusaidia shughuli za taasisi hiyo.
Amesema,hatua hiyo imetokana na uelewa wa Serikali kwamba vijana wanahitaji rasilimali za kifedha ili kubadilisha ndoto na mawazo yao kuwa miradi yenye tija.
“Tunachukua maamuzi haya kwa sababu tunatambua kuwa vijana wanahitaji fedha ili kutekeleza ndoto na miradi yao,”amesema.
Rais Chapo amewataka vijana kuchangamkia fursa hizo na kutumia mitaji watakayopewa katika shughuli za uzalishaji, ubunifu na ujasiriamali zitakazochangia maendeleo ya Taifa.
Vijana ni rasilimali ya kimkakati
Akizungumza katika mkutano huo, Rais Chapo amewataja vijana kuwa rasilimali kuu ya kimkakati ya Msumbiji, akisisitiza kuwa uhuru wa kisiasa uliopatikana nchini humo unapaswa sasa kubadilishwa kuwa ustawi na uhuru wa kiuchumi.
Amesema, jukumu la vijana ni kuzalisha mali, kuunda ajira, kuzalisha maarifa, kufanya ubunifu na kushiriki kikamilifu katika kujenga Msumbiji yenye maendeleo zaidi.
Kwa mujibu wa Rais huyo, utekelezaji wa dhamira hiyo ni sehemu ya safari ya kufikia uhuru wa kiuchumi wa Msumbiji.
Aidha, ametaja programu mbalimbali za Serikali zinazolenga kuwawezesha vijana zikiwemo FDEL, Acredita Emprega, Eu Sou Capaz, mradi wa Terra Infraestruturada pamoja na mipango ya kuwapatia wanafunzi wa vyuo vikuu kompyuta.
Awasihi vijana kudumisha umoja na amani
Rais Chapo pia amewataka vijana kutumia tofauti zao kama nguvu ya kujenga Taifa, akisisitiza umuhimu wa kuweka maslahi ya pamoja mbele.
Amesema, kile kinachowaunganisha wananchi kinapaswa kuwa kikubwa zaidi kuliko tofauti zinazowatenganisha.
Aidha, amesisitiza nafasi ya vijana wanaohudumu katika vyombo vya ulinzi na usalama katika mapambano dhidi ya ugaidi mkoani Cabo Delgado, akieleza kuwa hakuna maendeleo bila amani na usalama.
Kwa upande wake, Waziri wa Vijana na Michezo, Caifadine Manasse amemshukuru Rais Chapo kwa kuhudhuria mkutano huo licha ya majukumu yake mengine, akisema uwepo wake ni ishara ya kipaumbele anachokipa Serikali kwa vijana.
Mkutano huo umewakutanisha vijana kutoka mikoa mbalimbali ya Msumbiji kwa ajili ya kujadili changamoto na fursa zinazowakabili, pamoja na kutoa mapendekezo ya namna ya kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya Taifa.
Rais Chapo amehitimisha hotuba yake kwa kuwataka vijana kufanya kazi kwa bidii, kufanya ubunifu na kuendelea kujifunza na kuongeza ujuzi, akisisitiza kuwa hatua hizo ni muhimu katika kuharakisha maendeleo ya nchi.
Mradi wa Moz Community wazinduliwa
Katika ziara hiyo, Rais Chapo pia alizindua Moz Community Project unaolenga kuimarisha mshikamano wa kijamii, kupanua fursa za ajira na ushirikishwaji wa kiuchumi, pamoja na kuboresha upatikanaji wa miundombinu inayostahimili mabadiliko ya tabianchi.
Mradi huo unalenga kutekelezwa katika mikoa ya Cabo Delgado, Nampula na Niassa ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuongeza fursa za kiuchumi na kuimarisha ustahimilivu wa jamii katika maeneo hayo.(NA)

