Msumbiji yaanza utafiti wa siku 42 kuchunguza rasilimali za baharini

NA DIRAMAKINI

TAASISI ya Kitaifa ya Bahari ya Msumbiji (INAMAR) imekagua na kuipa leseni ya utafiti wa kisayansi meli ya Norway Dr.Fridtjof Nansen inayotarajiwa kufanya utafiti wa siku 42 katika maeneo ya bahari ya Msumbiji.
Utafiti huo unalenga kutathmini hali na uendelevu wa rasilimali za uvuvi ikiwemo ukubwa wa samaki waliopo, pamoja na kuchunguza mifumo ya ikolojia ya baharini katika maeneo mbalimbali ya mwambao wa Msumbiji.

Ukaguzi wa meli hiyo pamoja na uhakiki wa nyaraka ulifanywa na timu ya INAMAR iliyoongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukaguzi wa Bahari, Acácio Beleza akifuatana na Mkuu wa Usafiri wa Baharini wa Utawala wa Bahari wa Maputo, Daniel Ndeco.

Ujumbe huo ulipokelewa na Nahodha wa meli hiyo, Tommy Seeffensen ambaye aliwaongoza maofisa hao katika ziara ya kukagua sehemu mbalimbali za meli kabla ya kuanza kwa shughuli za utafiti.

Utafiti huo umefadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa idhini ya Serikali ya Msumbiji na unahusisha jumla ya wataalamu 18 wa sayansi watakaokuwa ndani ya meli hiyo wakati wa safari ya utafiti.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maofisa wa INAMAR wataambatana na msafara huo ili kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu za baharini zinazotumika nchini humo.

Aidha, ushiriki wa INAMAR unalenga kufuatilia utekelezaji wa kanuni za usimamizi endelevu wa rasilimali za baharini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uchumi wa buluu nchini Msumbiji.

Wakati huo huo, Hifadhi ya Taifa ya Maputo imetoa taarifa kwa umma kuhusu uwepo wa meli hiyo katika pwani ya hifadhi hiyo, ikieleza kuwa meli hiyo inafanya shughuli za utafiti kwa kushirikiana na Taasisi ya Oceanografia ya Msumbiji (InOM).

Hifadhi hiyo imewataka watalii, jamii za maeneo ya pwani,wavuvi na watumiaji wengine wa fukwe na maeneo ya bahari kutokuwa na hofu iwapo wataiona meli hiyo katika maeneo yao.
Picha zote na INAMAR.

Imesisitiza kuwa,uwepo wa Dr. Fridtjof Nansen katika maeneo hayo unahusiana na shughuli za utafiti wa kisayansi na si jambo la kutishia usalama wa wananchi au shughuli zao za kawaida.

Utafiti huo unatarajiwa kutoa taarifa muhimu kuhusu hali ya rasilimali za baharini na mifumo ya ikolojia katika mwambao wa Msumbiji, ambazo zinaweza kusaidia katika kupanga na kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali hizo kwa manufaa ya uchumi na jamii zinazotegemea bahari.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here