MV Liemba yafanyiwa majaribio baada ya ukarabati

KIGOMA-Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema Serikali imekamilisha hatua muhimu ya kurejesha huduma za meli ya MV Liemba baada ya kufanyiwa majaribio majini katika Bandari ya Kigoma, hatua inayolenga kuhakikisha meli hiyo inaanza tena kutoa huduma kwa wananchi wa ukanda wa Ziwa Tanganyika.
Profesa Mbarawa amesema hayo leo Jumamosi Agosti 15, 2026 akiwa mkoani Kigoma kushuhudia MV Liemba ikifanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza kuingia majini.

Amesisitiza kuwa, ukarabati wa MV Liemba ni matokeo ya jitihada za muda mrefu za Serikali za kutafuta mkandarasi kuanzia mwaka 2019 hadi 2022, ambapo mwaka 2023 chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mkataba ulisainiwa kwa ajili ya kufanya ukarabati mkubwa wa meli hiyo.

Amesema takribani Shilingi bilioni 34 zimetumika katika ukarabati huo, ambao umeifanya MV Liemba kubadilika kwa kiwango kikubwa, ikiwemo kufungwa injini mbili mpya, jenereta tatu mpya, vifaa vipya vya uendeshaji, maeneo mapya ya abiria pamoja na mbao mpya za deki.

Waziri Mbarawa ameongeza kuwa, mifumo na vifaa muhimu vya meli hiyo vimeboreshwa na kuwekwa kwa ubora unaohitajika, huku vifaa vya akiba vikiwa vimeandaliwa ili kuhakikisha huduma inaendelea kwa ufanisi.

Ameeleza kuwa, kutokana na ukarabati huo pamoja na matengenezo ya kawaida, MV Liemba inatarajiwa kuendelea kufanya kazi kwa angalau miaka 50 ijayo au zaidi.
Amesema kwa sasa meli hiyo ipo kwenye hatua ya majaribio ya kwanza majini (lake trials), ambapo wataalamu wanakagua utendaji wa injini, kasi, uwezo wa kusimama, uimara wa meli majini (stability) pamoja na mifumo ya dharura kabla ya kufanyiwa ukaguzi na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa ajili ya kupata kibali cha kuanza safari.

Profesa Mbarawa amesema endapo hatua zote zitakamilika kama ilivyopangwa, wananchi wa Tanzania na nchi jirani zinazotumia ukanda huo wataanza kutumia rasmi huduma za MV Liemba kuanzia Septemba Mosi, 2026..

Majaribio hayo ya majini ni hatua muhimu ya kuthibitisha usalama na utayari wa meli kabla ya kuanza kutoa huduma rasmi.
Kupitia majaribio hayo, wataalamu wanathibitisha uwezo wa meli kusafiri, kugeuka, kusimama na kufanya taratibu za dharura kwa usalama, huku mifumo ya uendeshaji ikiwemo injini kuu, gearbox, propeller, jenereta na mifumo mingine ikipimwa katika viwango tofauti vya mzigo na kasi.

Aidha, majaribio hayo yanahusisha ukaguzi wa mifumo ya uelekezi (steering system), vifaa vya mawasiliano na uelekezaji kama radar, GPS, AIS, dira na redio, pamoja na mifumo ya usalama na dharura ikiwemo vizima moto, alarm, jenereta za dharura na vifaa vya kuokoa maisha.

Hatua hiyo husaidia kubaini mapema changamoto zozote za kiufundi kama mtikisiko, joto kupita kiasi, uvujaji au hitilafu za mifumo kabla meli haijaingia kwenye huduma.
Majaribio hayo pia yanathibitisha ubora wa kazi iliyofanywa katika ukarabati wa meli hiyo na kuhakikisha kuwa inakidhi viwango vilivyowekwa pamoja na masharti ya kisheria yanayotakiwa kabla ya kutolewa vyeti vya kuanza safari.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here