Nchi za Pembe ya Afrika zaimarisha ushirikiano kukabiliana na uhalifu Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden

NA DIRAMAKINI

MAAFISA usalama kutoka Somalia, Ethiopia, Yemen na Djibouti wamekutana jijini Nairobi, Kenya katika mazungumzo ya kikanda yaliyolenga kuimarisha utekelezaji wa sheria baharini katika Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden, huku nchi hizo zikikabiliwa na vitisho vinavyovuka mipaka ya kitaifa.
Picha na Mtandao.

Mkutano huo wa siku mbili umefanyika wiki hii na kuandaliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) kwa ushirikiano na Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Kimataifa la Polisi (INTERPOL), Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini (IMO) na Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo (IGAD).

Lengo kuu lilikuwa kuimarisha mifumo ya kubadilishana taarifa, uratibu wa operesheni na ushirikiano baina ya taasisi za usalama na mamlaka za baharini katika kukabiliana na vitisho vinavyoathiri usalama wa majini katika ukanda huo.

Mkutano huo umefanyika wakati kukiwa na wasiwasi unaoongezeka kuhusu usalama wa njia za majini katika Mashariki ya Kati, hali ambayo maafisa wamesema,inaweza kuwa na madhara ya moja kwa moja kwa usalama wa Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden.

Abdurrahim Muhammad Ali kutoka Mamlaka ya Baharini ya Djibouti amesema,mabadiliko ya kiusalama katika maeneo mengine ya Mashariki ya Kati yanaweza kuwapa nafasi wahalifu wa baharini kurejea na kuongeza mashambulizi katika Ukanda wa Ghuba ya Aden.

Amesema,mashambulizi yanayoathiri uhuru wa usafiri wa meli katika Mlango wa Hormuz yanaweza kuwa na athari kwa usalama wa baharini katika Ghuba ya Aden, kwa kuwa uwepo na umakini wa vikosi vya majini duniani unaweza kuelekezwa katika maeneo mengine yenye migogoro.

“Unapozungumzia vitisho, mashambulizi ya sasa dhidi ya uhuru wa usafiri katika Mlango wa Hormuz yanaathiri Ghuba ya Aden kwa sababu yanaathiri usalama wa baharini.

"Maharamia hutumia fursa hii na usumbufu wa vikosi vya majini duniani kufanya mashambulizi zaidi katika eneo hili, kwa sababu wanajua kila mtu anaangalia upande mwingine,”amesema Abdurrahim Muhammad Ali.

Ikumbukwe kuwa,Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden ni miongoni mwa njia muhimu zaidi za usafirishaji wa majini duniani, zikiunganisha uchumi wa nchi za eneo hilo na masoko ya kimataifa.

Usalama wa njia hizo una umuhimu mkubwa kwa biashara ya kimataifa kutokana na kiasi kikubwa cha bidhaa kinachopita katika ukanda huo.

Kwa hiyo, usumbufu wowote wa usafirishaji unaweza kuongeza gharama za usafirishaji na bima, kuchelewesha mizigo na kuathiri minyororo ya usambazaji bidhaa katika maeneo yaliyo mbali na Pembe ya Afrika.

Mostafa Elbanna ambaye ni Mratibu wa Kikanda wa UNODC kwa Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden chini ya Mpango wake wa Kimataifa wa Kupambana na Uhalifu Baharini amesema,ukanda huo unakabiliwa na changamoto nyingi zinazohusiana kwa karibu.

Elbanna amesema,mazingira hayo yanaifanya iwe muhimu kwa taasisi za utekelezaji wa sheria na mamlaka nyingine zinazohusika na usalama baharini kukutana, kubadilishana uzoefu na kutafuta njia za pamoja za kukabiliana na changamoto hizo.

“(Huu ni wakati mzuri) wa kuwa na mijadala na mazungumzo ya aina hii na taasisi mbalimbali pamoja na vyombo vya utekelezaji wa sheria ili kujadili changamoto zao, lakini pia namna ya kusonga mbele linapokuja suala la usalama baharini,”amesema.

Miongoni mwa masuala yaliyopewa uzito katika mkutano huo ni uharamia, uvuvi haramu, usafirishaji haramu wa binadamu, usafirishaji wa wahamiaji kwa njia zisizo halali pamoja na biashara ya dawa za kulevya.

Aidha,maafisa wamesema changamoto hizo haziwezi kushughulikiwa kwa ufanisi na nchi moja pekee, kwa kuwa wahalifu hutumia mipaka ya kimataifa na mapengo ya ushirikiano wa kiusalama kutekeleza shughuli zao.

Ingawa kiwango cha uharamia katika ukanda huo kimepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na kile kilichoshuhudiwa zaidi ya muongo mmoja uliopita, Elbanna amesema, nchi za eneo hilo sasa zina uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na vitisho hivyo.

Ametaja kuimarika kwa utekelezaji wa sheria, ukusanyaji bora wa taarifa na takwimu,pamoja na kuongezeka kwa ushirikiano wa kikanda kuwa miongoni mwa hatua zilizosaidia kuimarisha uwezo wa nchi kukabiliana na uhalifu baharini.

Hata hivyo, maafisa wamesisitiza kuwa, kupungua kwa uharamia hakumaanishi tishio hilo limeondoka kabisa, hasa katika mazingira ambayo mivutano ya kijeshi na kisiasa katika Mashariki ya Kati inaweza kubadili kwa haraka hali ya usalama katika njia za majini.

Kwa Ethiopia, ambayo haina mwambao wa bahari, usalama wa baharini una umuhimu mkubwa wa kiuchumi kwa sababu sehemu kubwa ya biashara yake ya kimataifa hupitia katika nchi jirani ya Djibouti.

Kapteni Kibru Mesfin wa Mamlaka ya Baharini ya Ethiopia amesema,usalama wa njia za majini ni muhimu kwa kuhakikisha biashara ya nchi hiyo inaendelea bila vikwazo.

Amesema,usumbufu katika njia za usafirishaji baharini unaweza kuongeza gharama za usafirishaji na bima, kuchelewesha uingizaji wa bidhaa muhimu na kupunguza uwezo wa nchi kuuza bidhaa zake nje.

Madhara hayo amesema, yanaweza hatimaye kuongeza mzigo kwa wafanyabiashara na watumiaji, huku yakipunguza ufanisi wa shughuli za kiuchumi zinazotegemea biashara ya kimataifa.

Afisa huyo ametoa wito wa kuimarishwa kwa uhusiano baina ya mamlaka za baharini, walinzi wa pwani na vyombo vya utekelezaji wa sheria katika nchi za ukanda huo ili kuhakikisha biashara inaendelea kwa usalama na bila usumbufu usio wa lazima.

Aidha,amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mifumo iliyoratibiwa na inayofanana ya kubadilishana taarifa za baharini kati ya nchi jirani, zikiwamo Djibouti, Yemen na Somalia.

Mesfin amesema, kuanzishwa kwa Kituo cha Kitaifa cha Taarifa za Baharini nchini Ethiopia, sambamba na kuimarishwa kwa miunganiko yake na mifumo ya taarifa ya kikanda, kungewezesha mamlaka kupata taarifa kwa wakati na kufanya maamuzi sahihi zaidi kuhusu usalama baharini.

Kwa upande wa Djibouti maafisa wamesema, nchi hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazofanana na zile zinazowakabili majirani zake.

Ali ametaja ugaidi wa baharini, uvuvi haramu, uporaji, biashara haramu ya binadamu, uhamiaji usio wa kawaida na magendo kuwa miongoni mwa vitisho vinavyohitaji uangalizi mkubwa.

Pia,amesema kwa kuwa changamoto hizo zinafanana katika nchi mbalimbali, suluhisho lake linahitaji ushirikiano wa karibu na wa vitendo badala ya kila nchi kushughulikia tatizo lake peke yake.

“Matokeo ya vitendo ni kuwa karibu zaidi na kubadilishana taarifa kutoka Yemen, Somalia na Ethiopia.Tunakabiliwa na changamoto zilezile,”amesema.

Vilevile,washiriki wa mkutano walijadili pia namna ya kuboresha uelewa wa matukio yanayotokea katika maeneo ya baharini, unaojulikana kitaalamu kama maritime domain awareness, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiutendaji na kuweka mifumo bora zaidi ya kukabiliana na matukio ya kiusalama yanapotokea baharini.

Hatua hizo zinatarajiwa kusaidia mamlaka kutambua vitisho mapema, kubadilishana taarifa kwa haraka na kuratibu hatua za pamoja wakati wa matukio ya dharura.(NA)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here