NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema,Tamasha la Usiku wa Kizimkazi ni jukwaa muhimu la kuenzi na kuendeleza utamaduni wa Zanzibar huku likitoa fursa za kukuza utalii,uwekezaji na shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Dkt.Mwinyi amesema hayo baada ya kuhudhuria Tamasha la Usiku wa Kizimkazi lililofanyika usiku wa Agosti 13,2026 huko Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema,tamasha hilo limeendelea kuwa sehemu muhimu ya kuitangaza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, kwa kuunganisha utamaduni, sanaa,utalii na fursa za kiuchumi zinazoweza kuwanufaisha wananchi.
Kwa mujibu wa Dkt. Mwinyi, matukio ya aina hiyo yana nafasi kubwa katika kuendeleza urithi wa taifa, kuongeza mvuto wa maeneo ya utalii na kufungua fursa kwa wananchi kushiriki katika shughuli za kiuchumi zinazotokana na utalii na sekta nyingine zinazohusiana nao.
Aidha, Rais Mwinyi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza tamasha hilo, pamoja na wananchi,wadau na washiriki wote waliochangia kufanikisha tukio hilo.
Amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuyaunga mkono matukio yanayolenga kuimarisha utamaduni na utalii, akieleza kuwa sekta hizo ni miongoni mwa maeneo muhimu katika kukuza uchumi na kuongeza fursa kwa wananchi.
Tamasha la Kizimkazi limekuwa miongoni mwa matukio yanayovuta washiriki na wageni mbalimbali, likitoa nafasi ya kuonyesha utajiri wa utamaduni, sanaa na vivutio vya Zanzibar, sambamba na kutangaza fursa za uwekezaji na utalii.













