ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa Sekta Binafsi kushiriki katika ujenzi wa makaazi bora na miradi ya uwekezaji inayochochea ukuaji wa uchumi na kutoa fursa za ajira kwa wananchi.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Agosti 13,2026 wakati akizindua na kukagua Mradi wa Makaazi wa Amani Residency uliopo Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, ikiwa ni sehemu ya matukio ya Tamasha la Kizimkazi 2026.Amepongeza Bopar Enterprises Ltd na Mohammedi Builders Ltd kwa utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa uwekezaji huo utaongeza upatikanaji wa makaazi bora, fursa za ajira na biashara, pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi na utalii Kizimkazi na Mkoa wa Kusini kwa ujumla.
Amesema,Serikali itaendelea kuhamasisha ushiriki wa Sekta Binafsi na taasisi za fedha katika sekta ya makaazi, sambamba na kuimarisha miundombinu ya msingi ikiwemo barabara, maji, umeme na mawasiliano.Mradi wa Amani Residency uliojengwa katika eneo la ekari 11, una jumla ya nyumba 82, zikiwemo villa 18 na apartment 64, pamoja na huduma mbalimbali za kibiashara, burudani na mapumziko.
Mmiliki wa mradi huo, Bw. Said Bopar amesema, utekelezaji wake umewezeshwa kwa mkopo kutoka Benki ya CRDB unaofikia asilimia 70 ya gharama za mradi, akisisitiza umuhimu wa taasisi za fedha katika kuwezesha uwekezaji wa Sekta Binafsi.
Tags
Amani Residency Kizimkazi
Bopar Enterprises
Dkt.Hussein Ali Mwinyi
Habari
Said Bopar
Zanzibar News








