DAR-Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Mhe. Albert Chalamila amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa eneo la Toangoma Wilaya ya Temeke wenye mgogoro wa ardhi wa muda mrefu na Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF) ambapo ametoa muda wa wiki moja kukaa na NSSF ili kupata muafaka wa mgogoro huo kabla ya kwenda kufanya mkutano wa kuhitimisha mgogoro huo.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika kwenye eneo la Toangoma Temeke jijini humo RC Chalamila baada ya kusikiliza pande zote za mgogoro huo ambao ni wananchi na shirika la NSSF pamoja na upande wa ofisi ya kamishina wa ardhi amesema amejiridhisha kuwa eneo hilo mmiliki wake ni shirika la NSSF.
RC Chalamila amesema amepokea maombi ya wananchi wa Toangoma ambao wameomba shirika hilo ambalo liliamua kuwauzia wananchi ardhi hiyo kwa shilingi elfu 15 kwa mita za mraba kwa eneo la Malela na shilingi elfu 25 kwa mita ya mraba kwa eneo la Mwapemba ambapo wananchi wameomba kuuziwa kwa shilingi elfu tano kwa mita za mraba pamoja na kuongezewa muda wa kulipa.
Aidha,Chalamila amesema katika kipindi hicho ambacho amekusudia kukutana na wadau wanaohusika na mgogoro huo wananchi hao wasisumbuliwe na baada ya muda huo wa siku saba atakwenda kumaliza mgogoro huo na kwamba hata muda wa awali uliotolewa na NSSF kwa wananchi kupitia ardhi hiyo umefutwa ili waje na mpango mpya.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa ardhi Mkoa wa Dar es Salaam Rehema Mwinuka amethibitisha kuwa eneo hilo ni mali ua shirika la hifadhi za jamii NSSF huku Meneja miliki kutoka shirika la NSSF akieleza kuwa shirika baada ya kuona eneo lao limevamiwa waliamua kuwauzia eneo hilo kwa shilingi elfu 15 kwa mita ya mraba kwa eneo la Malela na shilingi elfu 25 kwa eneo la Mwapemba.
Awali, wananchi hao wenye mgogoro na shirika la hifadhi za jamii la MSSF wamemuomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Albert Chalamila kuwasaidia ili shirika hilo liwauzie eneo hilo kwa gharama rafiki ya shilingi elfu tano kwa mita ya mraba badala ya shilingi elfu 15 hadi elfu 25 kwa mita ya mraba kama walivyotaka NSSF kwani wao waliuziwa viwanja vya eneo hilo kwa kufuata taratibu wakishirikisha uongozi wa mtaa.
Aidha, wananchi hao wamemuomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwasaidia ili shirika hilo liwape muda mrefu wa kulipia wa kuamzia miaka minne hadi 10 badala ya muda mfupi wa miezi mitatu iliyotolewa na shirika hilo la NSSF kutokana na hali zao duni za maisha
Kwa mujibu wa taarifa iliyopo kwenye eneo hilo wananchi wengi waliingia kwenye maeneo hayo kwa zaidi ya miaka 16 iliyopita wakiuziwa ardhi kupitia ofisi za serikali ya mitaa yao na waliamini kiwa eneo hilo si mali ya NSSF.
Tags
Albert Chalamila
Dar es Salaam City
Dar es Salaam Region
Habari
Mgogoro wa Ardhi
NSSF Tanzania
Toangoma Temeke




