Serikali kutenga Shilingi bilioni 5 kujenga makazi ya kisasa ya wazee

DODOMA-Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,Mhe.Dkt. Dorothy Gwajima amesema, Serikali imetenga Shilingi bilioni 5 katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya ujenzi wa Makazi ya Kisasa ya Wazee katika kanda mbili nchini, yatakayotoa huduma jumuishi za ustawi wa jamii kwa wazee na jamii kwa ujumla.
Dkt.Gwajima ameyasema hayo Agosti 17, 2026 wakati akiwasilisha taarifa kuhusu hali ya utoaji wa huduma katika Makazi ya Wazee kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, akieleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha ulinzi, matunzo, utu na ustawi wa wazee nchini.

Amesema, hatua hiyo inazingatia ongezeko la idadi ya wazee nchini, ambapo kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, idadi yao imeongezeka kutoka 2,507,568 mwaka 2012 hadi 3,406,464 mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 35.8.

Aidha, amesema Wizara inasimamia Makazi 13 ya Wazee yenye jumla ya wahudumiwa 236, wakiwemo wanaume 142 na wanawake 94, huku ikiratibu Makazi 16 yanayoendeshwa na taasisi binafsi na mashirika ya dini yenye wahudumiwa 237.
Amesema, Serikali inaendelea kuhakikisha wazee wanapata huduma za msingi zikiwemo matibabu, lishe bora, afya ya akili, ulinzi na huduma nyingine za ustawi wa jamii.

Dkt. Gwajima amesema,katika mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara imetenga Shilingi milioni 400 kwa ajili ya ukarabati wa Makazi ya Wazee Misufini mkoani Tanga, Bukumbi Mwanza, Kiilima Kagera na Nyabange Mara.

Amesisitiza kuwa,pamoja na hatua hizo, Serikali itaendelea kutekeleza mikakati ya kuimarisha huduma za wazee na kuhakikisha wanapata matunzo, ulinzi, utu na huduma zinazostahili.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii,Mhe. Hawa Mchafu ameipongeza Wizara kwa hatua inazoendelea kuchukua katika kuboresha huduma na mazingira ya Makazi ya Wazee nchini.
Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuongeza kasi katika utekelezaji wa mikakati hiyo na kuhakikisha inaonesha matokeo yanayoonekana katika kuboresha huduma, miundombinu, ustawi na maisha ya wazee.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,Ndugu Eliakimu Chacha Maswi amesema, Wizara imepokea maelekezo na ushauri uliotolewa na Kamati hiyo na itayafanyia kazi kwa kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa, ili kuhakikisha huduma zinazotolewa katika Makazi ya Wazee zinaendelea kuboreshwa, changamoto zilizobainishwa zinapatiwa ufumbuzi na wazee wanapata huduma bora zinazozingatia utu, heshima na ustawi wao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here