NA GODFREY NNKO
MKUTANO Mkuu wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 (Africa50 General Shareholders' Meeting-GSM) pamoja na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum), uliofanyika Agosti 5 na 6, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam umehitimishwa kwa mafanikio makubwa huku ukiacha kumbukumbu ya kudumu kwa washiriki kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika na duniani.
Mkutano huo, uliobeba kaulimbiu "Miaka Kumi ya Athari za Kiuchumi: Kutoka Kwenye Maono Hadi Utekelezaji" (A Decade of Economic Impact: From Ambition to Delivery), uliwakutanisha viongozi wa serikali, taasisi za fedha, wawekezaji, sekta binafsi na wataalamu wa miundombinu kujadili namna ya kuharakisha maendeleo ya Afrika kupitia uwekezaji katika miradi ya kimkakati.
Mbali na mijadala ya kitaalamu, washiriki walipata fursa ya kufurahia burudani zilizoonesha utamaduni na urithi wa Tanzania kupitia maonesho ya wasanii wa muziki na vikundi vya ngoma za asili, jambo lililoifanya Tanzania kuendelea kujitangaza kama kitovu cha utalii wa mikutano na matukio makubwa ya kimataifa.
Katika Jukwaa la Miundombinu Afrika, washiriki walijadili kwa kina mustakabali wa maendeleo ya miundombinu barani humo, wakisisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika sekta za usafiri, nishati, miundombinu ya kidijitali na miradi mingine yenye uwezo wa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha ushindani wa Afrika.
Wakati wa mjadala wa kufunga mkutano huo, wataalamu walieleza kuwa kutokana na mabadiliko yanayoendelea katika mazingira ya kisiasa na kiuchumi duniani, ni muhimu kwa Afrika kuimarisha uwezo wake wa kujitegemea, kutumia rasilimali zake kwa ufanisi na kuendeleza ajenda zake za maendeleo kwa ushirikiano wa karibu kati ya serikali, sekta binafsi na taasisi za kifedha.
Aidha, walisisitiza kuwa ushirikiano wa kikanda, ubunifu katika upatikanaji wa mitaji na utekelezaji wa miradi yenye tija ni nguzo muhimu katika kuifanya Afrika kuwa na uchumi imara na wenye ushindani duniani.
Kwa Tanzania, kuwa mwenyeji wa mkutano huo kumetoa fursa ya kipekee ya kutangaza vivutio vya utalii, mazingira rafiki ya uwekezaji pamoja na miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa nchini, hatua inayotarajiwa kuvutia mitaji zaidi kutoka ndani na nje ya bara la Afrika.
Washiriki pia walieleza kuwa,mikutano hiyo imefungua milango mipya ya ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji, huku ikiiweka Tanzania katika nafasi muhimu ya kuendelea kuwa kitovu cha majadiliano kuhusu maendeleo ya miundombinu na uchumi wa Afrika.
Pia,wamefurahia ukarimu wa Watanzania huku wakipongeza namna ambavyo wanaendelea kudumisha amani na mshikamano, jambo ambalo wamesema linapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa mataifa mengine ndani na nje ya Afrika.





























