Tanzania yaahidi ushirikiano wa kutosha kwa Africa50

DAR-Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi, Khamis Mussa Omar (MB) amesema kuwa, Tanzania itaendelea kushirikiana na Taasisi ya Africa50 ambayo imejijengea heshima kama taasisi inayoongoza Afrika katika kuandaa miradi, kuhamasisha uwekezaji na kufadhili miundombinu kupitia ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ili kufikia maendeleo endelevu.
Mheshimiwa Balozi Omar amesema hayo wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 (Africa50 General Shareholders' Meeting - GSM) pamoja na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum), unaofanyika tarehe 5 na 6 Agosti, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), Dar es Salaam ambao ulifunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alisema kuwa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, Africa50 imejipambanua kama Taasisi ya uwekezaji wa miundombinu Afrika katika uandaaji wa miradi, ukusanyaji wa mitaji ya uwekezaji na ushirikiano wa kimkakati, ikionesha kuwa taasisi zinazoongozwa na Waafrika zinaweza kufanikiwa kuandaa miradi yenye kuleta mabadiliko Afrika.

‘‘Kauli mbiu ya "Muongo mmoja wa Athari za Kiuchumi: Kutoka Kwenye Nia Mpaka Kwenye Utekelezaji," inatukumbusha kuwa maendeleo endelevu hayapatikani tu kwa kuwa na maono, bali kupitia ushirikiano thabiti kati ya Serikali, taasisi za kifedha za maendeleo, wawekezaji na sekta binafsi ili kubadilisha mawazo kuwa miradi yenye tija na fursa za kiuchumi za kudumu kwa watu wetu,’’ alisema Mhe. Balozi Omar.
Aidha, alisema kwa upande wa Tanzania, maendeleo ya miundombinu ikiwemo mitandao ya kisasa ya usafiri, nishati, kidijitali na vituo vya usafirishaji yanaendelea kuwa nguzo kuu ya ajenda ya Taifa ya kukuza viwanda na ajira na kuwa Tanzania itaendelea kuwa mwanahisa kwa kuwa ina imani na mfumo jumuishi wa Taasisi hiyo katika kuleta maendeleo endelevu.

‘‘Wakati Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaendelea kuongoza ajenda ya mabadiliko ya kiuchumi inayotokana na uwekezaji wa kimkakati wa miundombinu, mtengamano wa kikanda, ushirikishwaji wa sekta binafsi na mazingira bora ya uwekezaji ili kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya uwekezaji na ukuaji wa uchumi endelevu Tanzania itaendelea kuwa mwanahisa kwa kuwa ina imani na mfumo jumuishi wa Taasisi hiyo,’’alifafanua Mhe. Balozi Omar.

Alisema mkutano huo wa siku mbili unatoa fursa kwa viongozi wa Serikali, wawekezaji na taasisi za fedha kujadili mbinu mbadala za ufadhili na kujenga ushirikiano wa kimkakati kubaini suluhu kwa mahitaji ya kifedha ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya miundombinu itakayofungua fursa mpya za kiuchumi barani Afrika.
Mhe. Balozi Omar, aliishukuru Taasisi ya Africa50 kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano huo ikiwa ni ishara ya imani kubwa kwa Tanzania na uwezo wa ukanda wa Afrika Mashariki katika kukuza maendeleo, kuimarisha uunganishaji wa kikanda na kufanikisha ustawi wa pamoja Afrika.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Africa50, Bw. Alain Ebobisse, alisema kuwa Taasisi hiyo inapotimiza miaka kumi tangu kuanzishwa, inajivunia mafanikio iliyopata katika kuendeleza miundombinu Afrika ambayo ni msingi wa kuharakisha uwekezaji katika sekta za nishati, usafiri, miundombinu ya kidijitali, usalama wa miundombinu na mifumo ya fedha, kwa lengo la kuifanya Afrika kuwa kitovu cha uwekezaji wenye ushindani duniani.

Alisema kuwa katika kipindi cha muongo mmoja, Africa50 imetambulika duniani kwa kushiriki katika miradi 26 yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni moja katika nchi mbalimbali za Afrika ambapo kupitia Mfuko wa Africa50 Infrastructure Acceleration Fund, Taasisi hiyo imefanikiwa kukusanya zaidi ya dola milioni 300 kutoka kwa wawekezaji 26, ambapo wawekezaji 23 kati yao ni Waafrika, hatua inayothibitisha kuwa mtaji wa ndani una uwezo wa kuchochea maendeleo ya Afrika.
‘‘Kuelekea muongo ujao Africa50 itaendelea kuwa Taasisi imara itakayowezesha Afrika kufadhili miradi yake kwa kutumia rasilimali za ndani kwa kuongeza mtaji unaosimamiwa hadi kufikia dola za Marekani bilioni tano, hatua inayotarajiwa kuchochea zaidi ya dola bilioni 30 za uwekezaji kutoka sekta binafsi na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika sekta za nishati, uchumi wa kijani, usafiri na miundombinu ya kidijitali,’’ alisema Bw. Ebobisse.

Bw. Ebobisse alisisitiza kuwa ni wakati wa kutumia rasilimali za gesi asilia za Afrika kuinua uwekezaji katika nishati inayoweza kuendesha viwanda, kuongeza uzalishaji wa kilimo, kuchochea uongezaji thamani wa madini, pamoja na kuboresha sekta za afya na usafiri, hatua ambayo ni msingi wa mapinduzi ya viwanda na ukuaji endelevu wa uchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here