Waziri wa Fedha ashiriki Mjadala wa Ngazi ya Juu ukiangazia umuhimu wa urejeshaji na uwekezaji upya wa mali

DAR-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameshiriki katika Mjadala wa Ngazi ya Juu (High-Level Roundtable) uliojadili kwa kina umuhimu wa urejeshaji na uwekezaji upya wa mali (asset recycling) kama mojawapo ya mbinu ambazo bado hazijatumika ipasavyo katika kufadhili miradi ya miundombinu barani Afrika.
Mjadala huo umefanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, ukiwa sehemu ya Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa taasisi ya Africa50 pamoja na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Africa50 General Shareholders’ Meeting – GSM and Infra for Africa Forum). Mkutano huo umebeba kaulimbiu isemayo, “Miaka Kumi ya Mafanikio: Kutoka Maono hadi Utekelezaji (A Decade of Economic Impact: From Ambition to Delivery).”
Mjadala huo umehudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Serikalini na sekta binafsi, ambapo pamoja na masuala mengine, umeangazia namna Serikali zinavyoweza kuachilia mtaji wa umma uliokwama katika mali zilizokomaa na kuuelekeza upya katika vipaumbele vipya vya maendeleo, hususan miradi ya kimkakati ya miundombinu.

Miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu walioshiriki katika mjadala huo ni Waziri wa Nchi anayeshughulikia Fedha, Bajeti, Uchumi, Mipango na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Chad, Mhe. Tahir Hamid Nguilin; Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Carla Loveira; Waziri wa Nchi anayeshughulikia Uwekezaji wa Umma na Uhamasishaji wa Rasilimali wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Tesi Rusagara; Waziri wa Fedha na Masuala ya Uchumi wa Jamhuri ya Gambia, Mhe. Seedy K. M. Keita; pamoja na Waziri wa Mipango, Uwekezaji na Maendeleo ya Uchumi wa Somalia, Mhe. Abdirahman Haile.
Wengine ni pamoja na Waziri wa Uchumi, Fedha na Bajeti wa Jamhuri ya Guinea, Mhe. Mariama Ciré Sylla; Afisa Mtendaji Mkuu wa Africa50, Bw. Alain Ebobissé; Rais wa Kundi na Mkurugenzi Mtendaji wa TDB Group, Bw. Admassu Tadesse; Afisa Mtendaji Mkuu wa ATIDI, Bw. Manuel Moses; pamoja na viongozi wengine kutoka taasisi za fedha na miundombinu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here