NA DIRAMAKINI
AFISA Manunuzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, Juma Ibrahim Mvumi amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mbulu kwa tuhuma za rushwa na uhujumu uchumi.
Kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi namba 20357/2026 imefunguliwa Septemba 9,2026 mbele Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Mheshimiwa Erick Rwehumbiza.
Mshtakiwa anashtakiwa kwa makosa sita ya matumizi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 marejeo ya 2019 ikisomwa pamoja na aya ya 21 Jedwali la kwanza na vifungu vya 57 (1) na 60 (2) ya Sheria ya Uhujumu Uchumi, pamoja na Makosa ya Kupangwa [Sura ya 200] marejeo ya 2019.
Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), Bw. Amiri Addy ameieleza mahakama kuwa, mtuhumiwa huyo alikiuka kanuni za manunuzi pamoja na Miongozo ya force account katika kufanya manunuzi ya umma.
Ni katika kutekeleza mradi wa "SUSTAINABLE RURAL WATER SUPPLY AND SANITAZATION PROGRAM (SRWSSP)" uliokuwa unatekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kwa kumpendelea mzabuni DOMA ENTERPRISES kwa kumpatia tenda ya kusambaza vifaa vya ujenzi katika miradi hiyo yenye thamani ya Shilingi 31,217,920 bila kushindanishwa.
Mshtakiwa amesomewa hati ya mashtaka na amekana mokosa yote sita yanayomkabili.
Aidha, Mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili na kudeposit nusu ya pesa ya thamani ya kesi ambayo ni Shilingi 15,000,000 au kuwasilisha Hati ya Mali isiyohamishika iliyofanyiwa tathmini yenye thamani ya Shilingi 15,000,000, hivyo amepelekwa mahabusu.
Shauri limehairishwa hadi Septemba 17,2026 kwa ajili ya Hoja za awali (PH).