DODOMA-Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 2) wa Mwaka 2026 (The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No. 02) Bill, 2026) leo Septemba 2,2026 katika Mkutano wa Nne, Kikao cha Sita cha Bunge kilichofanyika bungeni jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha muswada huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Hamza S. Johari amesema kuwa,muswada unakusudia kufanya maboresho katika sheria kuu saba.
"Malengo ya marekebisho haya ni kuboresha utekelezaji wa masharti ya sheria husika na kuzifanya sheria hizi ziendane na wakati na kuleta tija kwa wananchi,"amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amezitaja Sheria zilizofanyiwa marekebisho ni pamoja na Sheria ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Sura ya 116, Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287, Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288 na Sheria ya Baraza la Usalama la Taifa, Sura ya 61.
Mheshimiwa Johari ameendelea kueleza kuwa, Sheria ya Mamlaka ya Nchi katika Umiliki wa Mali na Rasilimali Asilia, Sura ya 449, Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini, Sura ya 138, Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, Sura ya 283 nazo zimejumuishwa katika muswada huo.Katika hatua nyingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa,Serikali itaendelea kufanya maboresho katika sheria mbalimbali ili kuhakikisha kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatekekelezwa ipasavyo.
"Kwa niaba ya Serikali, niliahidi Bunge lako Tukufu kuwa,Serikali itaendelea kufanya maboresho ya sheria ili kuhakikisha kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu inatekekelezwa ipasavyo,"amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mara baada ya Bunge kupitisha muswada huo, utapelekwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kusainiwa na kuwa sheria kamili za nchi.
Tags
Bunge la Tanzania
Habari
Muswada wa Mabadiliko ya Sheria
Muswada wa Sheria Na.2 wa Mwaka 2026
Mwanasheria Mkuu wa Serikali





