EgyptAir yaanza safari za moja kwa moja kati ya Cairo na Zanzibar,ikiimarisha utalii na biashara

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Zanzibar imeendelea kuimarisha nafasi ya Zanzibar katika ramani ya utalii na usafiri wa anga duniani, baada ya Shirika la Ndege la Misri la EgyptAir kuanza rasmi safari za moja kwa moja kati ya Cairo na Zanzibar.
Ndege ya kwanza ya EgyptAir kutoka Cairo nchini Misri, iliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA) majira ya saa 11:00 alfajiri, ikiwa na jumla ya abiria 152, hatua iliyoweka rasmi msingi wa safari za moja kwa moja kati ya miji hiyo miwili.

Mapokezi ya safari hiyo ya kihistoria yalihudhuriwa na mgeni rasmi, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed pamoja na viongozi, wadau wa sekta ya usafiri wa anga na wawakilishi wa sekta ya utalii.

Kuanzishwa kwa safari hizo kunatarajiwa kuongeza fursa za usafiri kati ya Zanzibar na Misri, huku Cairo ikiwa ni miongoni mwa vituo muhimu vya usafiri wa anga vinavyounganisha Afrika na maeneo mbalimbali duniani.

Huduma hiyo mpya inatarajiwa pia kutoa msukumo kwa ukuaji wa utalii, biashara na uwekezaji Zanzibar, kwa kurahisisha usafiri wa moja kwa moja kwa wageni kutoka Misri, pamoja na wasafiri kutoka masoko mengine yanayounganishwa kupitia Cairo.

Ratiba iliyotangazwa na EgyptAir itaendesha safari hizo mara mbili kwa wiki, siku za Jumatatu na Jumamosi, kwa kutumia ndege aina ya Boeing 737-800.
Akizungumza katika hafla ya mapokezi ya safari hiyo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha na kupanua huduma za usafiri wa anga ili kuunga mkono ukuaji wa sekta ya utalii na uchumi wa Zanzibar.

Amesema, kuimarishwa kwa miundombinu na huduma za usafiri wa anga ni sehemu muhimu ya juhudi za kuifanya Zanzibar kuwa eneo linalofikika kwa urahisi zaidi na kuvutia watalii, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Aidha,kuwasili kwa EgyptAir Zanzibar kunaongeza mtandao wa safari za kimataifa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume na kuimarisha zaidi hadhi ya Zanzibar kama kituo muhimu cha utalii na usafiri katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Safari ya moja kwa moja kati ya Cairo na Zanzibar inachukua takribani saa tano na dakika 45, hivyo kuwawezesha wasafiri kutoka miji hiyo miwili kusafiri bila kulazimika kupitia kituo kingine cha ndege.

Upande wa Zanzibar kuongezeka kwa safari za moja kwa moja za kimataifa kunaweza kupanua wigo wa masoko ya utalii, kuongeza idadi ya wageni na kuchochea shughuli zinazohusiana na utalii, zikiwamo hoteli, usafirishaji, biashara na huduma nyingine za sekta hiyo.
Safari za EgyptAir kati ya Cairo na Zanzibar zinatajwa kuwa hatua nyingine muhimu katika kuimarisha muunganiko wa Zanzibar na dunia, huku zikifungua fursa zaidi za kukuza utalii, biashara na uwekezaji na kuifanya Zanzibar kuwa miongoni mwa maeneo yanayozidi kufikika katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here