NA DIRAMAKINI
KATIBU Mkuu wa Chama cha United Party for National Development (UPND) nchini Zambia, Batuke Imenda amewataka mawaziri kuendelea kushirikiana na miundo ya chama, akisema baadhi yao wamejikuta mitaani baada ya kupuuza chama kilichowaunga mkono hadi wakateuliwa serikalini.
Imenda alitoa kauli hiyo jijini Lusaka wakati Waziri wa Uchumi wa Kijani na Mazingira, Dkt.Gilbert Siame alipofanya ziara ya heshima katika Ofisi Kuu ya UPND iliyopo Anderson Kambela Mazoka House.
Amesema, baadhi ya mawaziri hukumbuka kurejea katika sekretarieti ya chama pale wanapohitaji uteuzi wa kugombea nafasi mbalimbali, hali ambayo kwa mujibu wake, imechangia baadhi yao kujikuta nje ya nafasi walizokuwa nazo.
“Baadhi ya mawaziri wanarudi katika sekretarieti ya chama pale wanapotaka uteuzi. Hii ni moja ya sababu inayowafanya baadhi yao kuwa mitaani,” alisema.
Bw.Imenda amesema,chama kinaendelea kuwa kiungo muhimu kati ya Serikali na miundo yake, akimtaja Dkt. Siame kuwa amefanya jambo la kutambua mchango wa chama katika kuunga mkono Serikali na uongozi wake.
Amesema,ziara kama hiyo si jambo linalofanyika mara kwa mara, hivyo akawataka mawaziri na makatibu wakuu kuendelea kushirikiana na chama na kutambua umuhimu wa miundo inayounga mkono utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Kwa upande wake, Dkt.Siame amesema, ameamua kutembelea sekretarieti ya chama kwa kutambua kwamba uteuzi wake kuwa waziri ulifanyika chini ya uongozi wa Rais Hakainde Hichilema na UPND.
Amesema,sera zinazotekelezwa na wizara yake zinaendana na ilani ya UPND, hivyo ni muhimu kwake kudumisha mazungumzo na viongozi wa chama pamoja na kutafuta ushirikiano na mawazo yao.
Dkt.Siame amesema, wizara yake itafanya kazi kwa mtazamo mpana huku ikizingatia uwazi, matumizi yenye tija ya fedha za umma, kutokomeza rushwa na kuongeza kasi katika utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya Serikali.
Naye Mwenyekiti wa Taifa wa UPND, Collins Maoma ameikaribisha ziara hiyo na kusema chama kiko tayari kumuunga mkono Dkt. Siame katika utekelezaji wa majukumu yake.
Bw.Maoma amesema, chama pia kiko tayari kushirikiana na wizara hiyo katika kuwafikia wananchi na vijana, kwa lengo la kuendeleza ajenda ya maendeleo ya Serikali.
Ziara ya Dkt.Siame katika sekretarieti ya UPND imefanyika muda mfupi baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Uchumi wa Kijani na Mazingira.(NA)
