Naibu Waziri wa Fedha ateta na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa (UN)

NEW YORK-Naibu Waziri wa Fedha,Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo ya kimkakati na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa (UN), New York nchini Marekani, Mhe. Balozi Togolani Mavura, mara baada ya kukamilika kwa Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Jukwaa la Kimataifa la Fedha za Mabadiliko ya Tabianchi (Private Climate Finance Community).
Mkutano huo ulioratibiwa na Baraza la Uchumi la Dunia (WEF) kama sehemu ya Mikutano ya Athari za Maendeleo Endelevu 2026 (SDIM26), ulifanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York, Marekani.

Mhe. Balozi Mavura ameeleza matokeo ya ushiriki wa Tanzania kwenye jukwaa hilo, akibainisha fursa za uwekezaji wa sekta binafsi za kimataifa zilizotengwa kwa ajili ya afua za mabadiliko ya tabianchi na miradi ya nishati safi ambapo Tanzania imefanikiwa kuweka wazi vipaumbele vyake katika kuvutia mitaji ya sekta binafsi ili kufadhili miradi endelevu inayotunza mazingira na kukuza uchumi wa kijani.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), alimpongeza Mhe. Balozi Mavura na Timu yake ya wanadiplomasia kwa kuendelea kuipeperusha vyema Bendera ya Tanzania katika majukwaa ya kimataifa akisisitiza kuwa Serikali imejipanga kutekeleza diplomasia ya kiuchumi na mazingira, na kuagiza kuwa matokeo ya mkutano huo yabadilishwe kuwa mipango kazi madhubuti itakayounganishwa na sekta za ndani ili fursa hizo ziwafikie wananchi kwa haraka.
Mhe. Munde alielekeza Wizara kuendelea kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Ubalozi wa Kudumu ya Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York ili kuhakikisha wawekezaji waliovutiwa wanaratibiwa vizuri na kupewa ushirikiano wa kutosha wanapoingia nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here