NA GODFREY NNKO
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametoa salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatia kifo cha mume wake, marehemu Hafidh Ameir Hassan kilichotokea leo Septemba 7,2026 katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Emilio Mzena,Zanzibar.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 7,2026 na Kaimu Mkurugenzi, Mawasiliano Ikulu ya Zanzibar,Bw.Raqey Mohamed
Kwa mujibu wa taarifa hiyo,Rais Dkt.Mwinyi amesema,amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba huo na kuungana na Rais Dkt. Samia, familia, ndugu, jamaa pamoja na wote walioguswa na msiba huo katika kipindi hiki cha majonzi.
Amesema, msiba huo ni mkubwa kwa familia na wote waliokuwa karibu na marehemu, hivyo amemuomba Mwenyezi Mungu amjaalie Rais Dkt. Samia pamoja na familia yake subira, nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu.
Marehemu Hafidh Ameir Hassan anatarajiwa kuzikwa leo Kizimkazi, Zanzibar katika maziko yatakayohuduriwa na familia, ndugu, jamaa, viongozi mbalimbali wa kitaifa pamoja na wananchi.
Rais Dkt.Mwinyi amemuomba Mwenyezi Mungu amsamehe na amrehemu marehemu Hafidh Ameir Hassan na amjaalie makaazi mema peponi.
Inna Lillahi wa Inna Ilayhi Raji'un.
Tags
Dkt.Hussein Ali Mwinyi
Dr Samia Suluhu Hassan
Habari
Hafidh Ameir Hassan
Salamu za Pole
Zanzibar News
