Serikali kumtua mama ndoo ya maji kichwani na kujenga Taifa lenye usalama wa maji

NA DIRAMAKINI

NI mkakati wa serikali katika kuhakikisha huduma ya maji inamfikia kila Mtanzania popote pale alipo. Jitihada hizo zinaanzia katika uwezo wa rasilimaliwatu, fedha na mwitikio wa wananchi katika kushirikishwa na kutoa mrejesho kuhusu mahitaji.
Taswira ya eneo la mradi wa mtambo wa kutibu majitaka eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam ikiwa ni moja ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhusu usafi wa mazingira na afya ya jamii ukiwa mtambo mkubwa na wa kisasa wa kuchakata majitaka ukanda wa Afrika Mashariki. Mradi unatekelezwa na Wizara ya Maji unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba,2026 na utanufaisha kaya zaidi ya 11,000 katika kata nne za Wilaya ya Kinondoni ambazo ni Kawe, Kunduchi, Mbezi Juu na Wazo.

Mapema kabisa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Bajeti ya Sekta ya Maji kwa mwaka wa fedha 2026/27 katika kipindi ambacho matarajio ya wananchi kuhusu huduma ya maji yameongezeka kwa kiwango kikubwa.

Kadiri uchumi unavyokua, idadi ya watu inavyoongezeka na shughuli za uzalishaji zinavyoongezeka, ndivyo umuhimu wa Sekta ya maji unavyozidi kuwa mkubwa kama moja ya chanzo muhimu katika kusukuma maendeleo ya taifa.

Umuhimu wa sekta hiyo kwa jamii, umeisukuma Serikali kutenga zaidi ya Shilingi trilioni 1.12 kwa Wizara ya Maji katika mwaka wa fedha 2026/27. Ni kiasi kikubwa zaidi kuwahi kutengwa katika historia ya Sekta ya Maji hapa nchini, ambapo hatua hiyo inaakisi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha huduma ya majisafi na salama inazidi kuimarika na kuwafikia wananchi wengi katika makazi yao.

Kwa wakazi wa vijijini na mijini, bajeti iliyotengwa sio jambo la mkusanyiko wa takwimu pekee. Ni bajeti inayobeba matumaini; ya mama anayelazimika kutembea nje ya makazi yake kutafuta huduma ya maji, mkulima anayehitaji uhakika wa maji kwa kazi ya uzalishaji, mwanafunzi anayehitaji utulivu kwa mazingira bora ya kujifunza na mwekezaji anayehitaji rasilimali ghafi za uhakika kuendesha shughuli zake za kiuchumi.

Maji ni Nguzo ya Uchumi na Maendeleo

Dunia ya leo, Sekta ya maji haisimami kama huduma ya maji bali ni nguzo muhimu inayochochea maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja na uchumi kwa ujumla.

Wizara ya Maji imejipambanua kwa utekelezaji wa kazi zake kwa kuzingatia misingi mikuu mitatu ambayo ni; usalama wa maji katika taifa, maji kwa ajili ya ukuaji wa uchumi na huduma endelevu za maji. Mwelekeo huu unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga taifa lenye uhakika wa maji kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa utunzaji wa vyanzo vya maji, miradi na ushirikishwaji wa wananchi.

Kwa mantiki hiyo, maji sio suala la matumizi ya nyumbani peke yake. Ni suala la uzalishaji wa chakula, maendeleo ya viwanda, uzalishaji wa nishati, afya ya jamii na ukuaji wa uchumi kwa ujumla. Hivyo, ndiyo maana bajeti ya mwaka 2026/27 imejengwa katika msingi wa kuimarisha usalama wa maji kwa muda mrefu badala ya kutanzua changamoto za muda mfupi peke yake.

Bajeti hii inaakisi safari ya mafanikio inayoendelea, takwimu zinaonesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika Sekta ya Maji ndani ya kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Mwaka 2006, upatikanaji wa maji vijijini ulikuwa wastani wa asilimia 50. Hadi kufikia Desemba 2025, kiwango hicho kiliongezeka hadi asilimia 85.2. Kwa upande wa maeneo ya mijini, huduma ya maji imeongezeka kutoka asilimia 73 mwaka 2006 hadi asilimia 92.5. Mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa miradi ya miradi ya maji iliyojengwa katika maeneo mbalimbali nchini kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji.

Aidha, bajeti ya Sekta ya Maji imeongezeka kwa kasi kutoka shilingi bilioni 310 mwaka 2007 hadi zaidi ya shilingi trilioni moja mwaka 2026. Ongezeko hilo limeiwezesha Serikali kuanzisha na kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ambayo hapo awali ilionekana kuwa ndoto.

Kukamilika kwa miradi ikiwemo ya Same-Mwanga-Korogwe, Mugango-Kiabakari-Butiama, Nzega-Igunga-Tabora, ujenzi wa Bwawa la Kidunda na kuanza kwa utekelezaji wa miradi ya Miji 28, Kiwira, Bwawa la Farkwa na mingine mingi ya kimkakati imekuwa sehemu ya mageuzi makubwa ya Sekta ya Maji nchini.

Nyota njema kwa Vijiji 1,575 vilivyobaki

Hatua iliyopigwa ni kubwa, na safari inaendelea. Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado ipo idadi ya vijiji 1,575 ambavyo havijafikiwa kikamilifu na miundombinu rasmi ya huduma za maji. Hiki ndicho mojawapo ya vipaumbele vikuu vya bajeti ya mwaka 2026/27 ambayo inaendelea kutukelezwa.

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewakaribisha wadau mbalimbali, ikiwamo sekta binafsi kushiriki kukamilisha kazi hii. Sera ya Maji 2025 imefungua milango kwa Sekta Binafsi kushiriki katika kufikisha huduma ya maji katika jamii..

Serikali imeweka lengo la kuhakikisha vijiji vyote vilivyobaki vinapata huduma ya maji kabla ya mwaka 2030. Katika mwaka mmoja wa bajeti , idadi ya vijiji 314 vinatarajiwa kufikiwa na huduma hiyo.

Kwa wananchi wa maeneo hayo, bajeti hii inawakilisha matumaini mapya ya kuondokana na uhaba wa muda mrefu kwa kutafuta maji. Ni matumaini ya kuokoa muda na kuongeza uzalishaji, kuboresha afya za familia na kuongeza fursa za maendeleo ya jamii na uchumi.

Miongoni mwa mipango mikubwa iliyobebwa na bajeti hii ni utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji. Mradi huu una lengo la kutumia vyanzo vikuu vya maji vya Tanzania ikiwemo maziwa, mito mikubwa na mabwawa kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi. Ni kutoa maji katika maeneo yenye wingi wa maji kufika katika maeneo yenye uhitaji zaidi kutokana na ukosefu wa vyanzo vya uhakika vya maji.

Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali kubwa za maji ikiwemo Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na mito mingi mikubwa. Kupitia gridi hiyo, maji yatatumika si kwa matumizi ya nyumbani pekee bali pia kwa kilimo, mifugo, viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji.

Kimsingi huu ni mradi wenye uwezo wa kubadilisha historia ya sekta ya maji nchini kwa kuunganisha maeneo yenye vyanzo vingi vya maji na maeneo yenye upungufu wa huduma hiyo. Kwa uchache ni fursa kubwa kwa vijana wanaopenda kujikita katika kilimo au ambao wanapenda kuongeza ukubwa wa kazi katika mzunguko mzima wa kilimo.

Ujenzi wa Mabwawa na Uvunaji wa Maji ya Mvua

Mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuathiri upatikanaji wa maji katika maeneo mengi duniani. Tanzania nayo imeathirika kupitia vipindi vya ukame na mabadiliko ya mifumo ya mvua. Kutokana na hali hiyo, bajeti ya mwaka 2026/27 imeweka mkazo mkubwa katika uvunaji wa maji ya mvua na ujenzi wa mabwawa ya kimkakati. Mabadiliko ya tabianchi yawe fursa zaidi, na sio kuwa chanzo cha majanga katiuka jamii nchini Tanzania.

Katika mwaka, Serikali imepanga kujenga na kukarabati mabwawa 33, kufanya usanifu wa mabwawa mapya 34 pamoja na kuchimba visima virefu 300 katika maeneo yenye uhaba wa vyanzo vya maji.
Taswira ya eneo la mradi wa mtambo wa kutibu majitaka eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam ikiwa ni moja ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhusu usafi wa mazingira na afya ya jamii ukiwa mtambo mkubwa na wa kisasa wa kuchakata majitaka ukanda wa Afrika Mashariki. Mradi unatekelezwa na Wizara ya Maji unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba,2026 na utanufaisha kaya zaidi ya 11,000 katika kata nne za Wilaya ya Kinondoni ambazo ni Kawe, Kunduchi, Mbezi Juu na Wazo.

Mkakati huo unalenga kuhakikisha maji yanayopatikana wakati wa masika yanahifadhiwa kwa matumizi ya kipindi cha kiangazi na kupunguza athari za ukame. Mabwawa haya yanahusisha ujenzi wa mabwawa makubwa ikiwamo Bwawa la Kidunda-Morogoro na Farkwa-Dodoma kwa lengo la kuimarisha uzalishaji wa maji.

Teknolojia na Ufanisi wa Huduma

Bajeti imeangaza mkazo katika matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza ufanisi wa huduma za maji. Mifumo ya kidijitali ya usomaji wa mita, usimamizi wa mitandao ya maji na matumizi ya Dira za malipo kabla vinatarajiwa kupunguza upotevu wa maji (NRW) na kuongeza mapato ya taasisi zinazotoa huduma ya maji katika jamii. Dira za malipo kabla zinaongeza uhudru wa mteja anayehudumiwa katika kizimba kuchukua maji kwa wakati anaopanga mwenyewe, na majumbani kujinunulia maji kwa kiasi anachohitaji.

Hatua hizo zinazochukuliwa ni kuhakikisha fedha zinazowekezwa zinatoa matokeo yanayokusudiwa na huduma ya maji kwa wananchi ikiimarika.

Kwa ujumla, bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka 2026/27 imebeba zaidi ya namba za fedha. Ni bajeti inayobeba matumaini ya mamilioni ya Watanzania wanaotegemea huduma ya maji kwa maisha yao ya kila siku. Ni bajeti inayolenga kujenga taifa lenye usalama wa maji, kuongeza uzalishaji katika uchumi, kuboresha afya za wananchi na kuimarisha ustawi wa jamii.

Kadri utekelezaji wake utakavyoendelea, Watanzania wanatarajia kuona matokeo halisi katika vijiji, mitaa, shule, hospitali na maeneo ya uzalishaji nchini kote. Kwa utekelezaji wa malengo bajeti hii ni moja ya nyenzo muhimu zaidi katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kisasa unaotegemea rasilimali za maji kama msingi wa maendeleo endelevu.

Kwa wananchi, ujumbe ni mmoja tu: maji ni maisha, na bajeti hii imebeba matumaini makubwa kwa mustakabali wa upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama pamoja na usafi wa mazingira kwa Watanzania, maeneo ya mijini na vijijini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here