Serikali yatoa onyo kali matumizi batili ya Kitambulisho cha Taifa

NA DIRAMAKINI

MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ametoa onyo kwa wananchi dhidi ya kukabidhi vitambulisho au namba zao za NIDA kwa watu wengine, akisema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia vitambulisho vya ndugu au marafiki kusajili laini za simu.
Pia, amewataka Watanzania ambao vitambulisho vyao vya Taifa vimekamilika, lakini hawajavichukua kwenda katika ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuvichukua, akisema utambulisho ni msingi wa kupata huduma kwa usalama na ufanisi katika Tanzania inayojenga uchumi wa kidijitali.

Msigwa onyo hilo ametoa Semptemba, 1 2026 wakati akitangaza kuanza rasmi kwa kampeni ya kitaifa ya “Septemba ya Utambulisho”, ambayo itafikia kilele Septemba 16, ikiwa ni Siku ya Utambulisho Duniani, huku shughuli za uhamasishaji, utoaji wa elimu na huduma za NIDA zikiendelea nchini kote hadi Septemba 30, 2026.

“Matumizi haya ya kutumia Kitambulisho cha Taifa cha mtu yanaweza kumwingiza mwenye kitambulisho katika matatizo ya kisheria endapo laini hiyo itatumika kufanya uhalifu,”amesema.

Amesema hadi sasa zaidi ya milioni 1.5 ya vitambulisho vya Taifa vilivyokamilika vilikuwa bado havijachukuliwa na wananchi, licha ya serikali kutumia fedha nyingi katika uzalishaji wake.

“Wananchi waliopokea ujumbe wa simu unaowaarifu kuwa vitambulisho vyao vimekamilika kwenda kuvichukua katika ofisi za NIDA zilizopo wilayani Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, NIDA imepiga hatua kubwa katika usajili na utambuzi wa watu, ambapo hadi Julai 2022 jumla ya watu 27,458,832 walikuwa wamesajiliwa, sawa na asilimia 87.26 ya watu wenye umri wa miaka 18 na kuendelea. Pia vitambulisho 21,526,585 vilikuwa vimezalishwa na zaidi ya milioni 20 kati yake vilikuwa vimegawiwa kwa wananchi.

Msigwa amesema, umuhimu wa utambulisho umeongezeka kutokana na kuunganisha mifumo ya serikali na sekta binafsi, ambapo hadi Agosti 2026 jumla ya taasisi 157, zikiwemo 72 za serikali na 85 za sekta binafsi, zilikuwa zimeunganishwa na mfumo wa NIDA.

“Mfumo huo unasaidia taasisi kuhakiki taarifa za watu wanaopata huduma na kupunguza uwezekano wa udanganyifu na matumizi ya taarifa zisizo sahihi,”ameongeza.

Katika hatua nyingine, Msigwa amesema serikali imeanza kuboresha teknolojia ya uchapishaji wa vitambulisho vya Taifa kwa kutumia teknolojia inayolenga kuongeza uimara na usalama wa taarifa zilizomo kwenye kadi.

Serikali pia inapanga kuwa na kadi zenye uwezo mkubwa zaidi wa kubeba taarifa za utambulisho zinazohusiana na huduma nyingine, hatua inayolenga kupunguza idadi ya vitambulisho ambavyo wananchi hulazimika kubeba.

Aidha, NIDA itaendelea kuboresha teknolojia ya utambuzi wa kibaiolojia kwa kutumia sura na mboni za macho ili kupanua uwezo wa kuwatambua watu ambao alama za vidole haziwezi kutumika kwa ufanisi.

Msigwa amewataka Watanzania, taasisi za umma, sekta binafsi na vyombo vya habari kuifanya Septemba kuwa mwezi wa kuongeza uelewa kuhusu umuhimu na matumizi sahihi ya utambulisho. “Kipo, Chukue, Kamilisha Safari Yako,” ndiyo kauli mbiu ya kampeni hiyo

Amesisitiza kuwa utambulisho si kadi pekee bali ni msingi wa huduma, usalama, uchumi na maendeleo ya taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here