NEW YORK-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, amesema Tanzania itaendelea kuimarisha urafiki na Marekani kwa kuweka mazingira rafiki kwa raia, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini humo.
Akizungumza katika hafla ya kila mwaka ya Marafiki wa Tanzania jijini New York, Marekani, Waziri Kombo amesema Tanzania inatoa visa kwa raia wa Marekani wanapowasili nchini, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuonesha urafiki na kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili.
Aidha, Waziri Kombo amesema Serikali iko tayari kuwasaidia wafanyabiashara na wawekezaji katika masuala yanayohusu kanuni, sera na taratibu, huku Wizara ya Mambo ya Nje ikiwa tayari kushughulikia changamoto zinazoweza kujitokeza.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Elsie Kanza, amesema hafla hiyo imelenga kuadhimisha urafiki, ushirikiano na ubia kati ya Tanzania na Marekani, pamoja na kuimarisha mahusiano yenye manufaa kwa pande zote.
Hafla hiyo imeandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye Ulemavu nchini Tanzania, Prof. Palamagamba Kabudi (Mb.); Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida; Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Dkt. Zeyana Abdallah Hamid (Mb.).



















