TEA yatenga Shilingi bilioni 1.3 kujenga hosteli za Chuo cha IPA kisiwani Pemba

UNGUJA-Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imetenga takribani Shilingi 1.3 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa hosteli katika Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar (IPA) Kampasi ya Pujini Pemba, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia chuoni hapo.
Fedha hizo zitatumika kutekeleza mradi huo baada ya TEA na IPA kusaini mkataba maalumu wa ushirikiano wa ujenzi wa hosteli hiyo, katika hafla iliyofanyika Septemba 8, 2026.

Mkurugenzi Mkuu wa TEA,Dkt.Erasmus Kipesha amesema, uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za mamlaka hiyo kufadhili miradi ya elimu yenye lengo la kuongeza ubora na upatikanaji wa elimu nchini.

Amesema, TEA kama taasisi ya Muungano ina wajibu wa kushiriki katika kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji, huku akiitaka IPA kuhakikisha mradi huo unaanza na kukamilika kwa wakati.
"Ni imani yangu kuwa mradi huu ukikamilika utaongeza ufanisi katika ujifunzaji na ufundishaji, lakini pia kuongeza uwezo wa chuo kutoa huduma kwa wananchi na kuimarisha huduma za mafunzo kwa maendeleo ya sekta ya elimu,”amesema Dkt. Kipesha.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa IPA,Dkt. Hamad Khamis Said amesema, kukamilika kwa hosteli hiyo kutasaidia kupunguza changamoto ya malazi kwa wanafunzi na kuwawezesha kutumia muda mwingi katika masomo.
Amesisitiza kuwa, mradi huo utakuwa na matokeo chanya katika maendeleo ya taaluma chuoni, pamoja na kuboresha mazingira ya watumishi wa umma wanaopata mafunzo katika taasisi hiyo.

Dkt. Said amesema, TEA imekuwa mdau muhimu katika kuboresha miundombinu ya chuo, akitaja ruzuku iliyotolewa na mamlaka hiyo katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya ukarabati wa maabara ya kompyuta pamoja na ununuzi wa kompyuta.

“Ujenzi wa bweni hili kwetu sisi ni wa thamani sana na utaacha kumbukumbu kwa vizazi vijavyo hata kama hatutakuwepo. Tunawashukuru sana TEA kwa kuendelea kuwa sehemu ya uboreshaji na maendeleo ya chuo chetu,” amesema Dkt. Said.

Mradi huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa Kampasi ya Pujini kutoa huduma bora za malazi na kwa ujumla kuchangia uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia na utoaji wa mafunzo katika Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here